Serikali imesema kuwa hakuna akiba ya fedha iliyowekwa katika mfuko maalum kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa kwa sababu deni hilo linajumlisha Deni la Serikali na Deni la Sekta Binafsi, lakini Serikali inalipa deni lake pekee bila kuhusisha deni la Sekta Binafsi.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa
Akijibu maswali ya Mbunge wa Mtambile Mhe. Masoud Abdallah Salim aliyetaka
kujua Deni la Taifa limefikia kiasi gani na namna mchanganuo wa fedha
zilizowekwa akiba kwa ajili ya kulipa deni
hilo ulivyo.
“Fedha kwa
ajili ya malipo ya Deni la Serikali inatengwa kwa kuzingatia taratibu za
kawaida za kibajeti kupitia Fungu 22, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Serikali
ilitenga kiasi cha Sh. trilioni 1.262 kwa ajili ya malipo ya deni la ndani na
Sh. bilioni 685.06 kwa deni la nje”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisema hadi kufikia Aprili 30,
mwaka huu Deni la Taifa limefikia Dola za Marekani milioni 26,161.02 sawa na
zaidi ya Shilingi trilioni 59.4
Akijibu
swali la nyongeza la Mbunge huyo aliyetaka kujua mkakati wa Serikali
kuhakikisha Deni la Taifa linahakikiwa ili kujua kama Serikali inakopesheka au
la, Dkt. Kijaji alilihakikishia Bunge kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, Deni la Taifa litahakikiwa kama nchi nyingine
zinavyofanya kwani mkataba wa kuhakiki
deni hilo upo kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali katika hatua za mwisho.
Waziri huyo alisema
kuwa Deni la Taifa ni himilivu na Serikali imekuwa makini katika ulipaji kwa
kuhakikisha inalipa kila mwezi madeni katika Taasisi zote ilizokopa hali
inayoifanya nchi kuaminika na Taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa
Aidha, Mhe.
Kijaji alifafanua kuwa fedha zote zinazokopwa zinapelekwa katika shughuli za maendeleo
ya kiuchumi ili kuendelea kuinua uchumi wa nchi hususani katika kipindi hiki
cha uchumi wa viwanda.

