Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kufika mbele ya Kamati ya Bunge, Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Januari 21 mwaka huu, kujibu tuhuma alizozitoa dhidi ya muhimili huo kuwa dhaifu.
Pia wito huo umemkumba Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee, ambaye naye ametakiwa kuripoti mbele ya kamati hiyo, Januari 22 mwaka huu, kuthibitisha madai yake aliyoyatoa kupitia mitandao ya kijamiii kuwa Bunge ni dhaifu.
Hayo ameyasema leo jijini Dodoma Spika Ndugai alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ameeleza kuwa kama CAG anasema Bunge ni dhaifu basi atakuwa mpotoshaji mkubwa.
“Bunge tumepokea kwa masikitiko kuhusu kauli ya CAG, aliyoitoa Marekani. Kauli hiyo imelenga kutoa picha kwamba ripoti zake hazifanyiwi kazi au akishazifikisha Bungeni kazi inakuwa imekwisha, jambo ambalo si kweli.
Aidha Spika Ndugai aliongeza kuwa CAG na maofisa wake wanaingia kwenye Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC).
Spika alifafanua kuwa ripoti hizo zikifika kwenye kamati hizo ambazo zinaongozwa na upinzani, muda wote maofisa wa CAG wanakuwepo kueleza mapungufu waliyoyabaini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Ndugai amesisitiza kuwa tangu serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, imekuwa ikipambana dhidi ya matumizi mbaya ya fedha za umma na hatua zimekuwa zikichukuliwa.
Kadhalika alibainisha namna ambavyo Bunge limefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka mitatu tangu serikali ya Rais Dk. John Magufuli, ilipoingia madarakani.
Spika ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), amesema kuwa mabadiliko makubwa kwenye usimamizi wa fedha za umma yamefanyika kwa ushauri wa Bunge na CAG, hivyo alishangazwa na hatua zipi ambazo CAG alitaka zichukuliwe.
“Alitaka hatua gani zichukuliwe?. Napeleka tahadhari kwa maofisa wa serikali na wananchi kutojaribu kulidhalilisha Bunge. Si kama Bunge halitaki kukosolewa lakini si kwa kulikosoa kwa matamshi ya dharau ambayo ameyatoa wakati akiwa nje ya nchi.
Ndugai alieleza: “Ni ustaarabu kutoisema nchi yako vibaya ukiwa nje ya nchi. Wapo watakaosema CAG ana uhuru kikatiba, lakini kwenye katiba hakuna aliyehuru bila kuwa na uwajibikaji.
Hata hivyo amesema kuwa ni vigumu kufanyakazi na mtu anayeliona Bunge dhaifu ambapo alimshauri CAG ajitathimini, kwani muhimuli huo hautokubali kudhalilishwa.

