Breaking News

Walimu waomba kuwe na somo la rushwa



Na. Ahmad Mmow,Nachingwea.

Katika harakati za kuzuia na kupambana na tatizo la rushwa nchini.Baadhi ya walimu katika wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi,wameiomba serikali kuingiza kwenye mtaala somo litakalozungumzia rushwa.

Hayo yalijiri juzi mjini Nachingwea kwenye ziara ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)na idara ya Uhamiaji katika baadhi ya shule za msingi zilizopo mjini humo.

Mwalimu kiongozi(mwalimu mkuu) wa shule ya msingi Ilulu,Sarah Chibwana alisema itakuwa vema kama kutakuwa na somo maalumu litakalofundisha mambo yanahusiana na rushwa.Kwani tatizo la rushwa nikubwa,inabidi lianze kufundishwa shuleni.

Alisema walimu wananafasi kubwa ya kuwaelimisha wanafunzi madhara ya tatizo la rushwa.Hivyo kama litafundishwa shuleni watakuwa wamewajengea msingi mzuri katika mapambano dhidi ya tatizo hilo.

Nae mwalimu Masoud Hassan ambae ni mwalimu kiongozi wa shule ya msingi ya Nachingwea,alisema TAKUKURU inajitahidi sana kutoa elimu shuleni.Ikiwamo kuanzisha klabu za kupambana na rushwa.Hata hivyo elimu hiyo haitoshi,hivyo kuna umuhimu wa kuingiza kwenye mtaala somo litakalozungumzia rushwa.

Mwalimu Masoud alisema madhara ya rushwa nimakubwa.Ikiwamo kukosekana uzalendo na uhasama katika jamii.Kwahiyo kuna umuhimu kwa watoto kujengewa msingi wa kuchukia rushwa.

Hata hivyo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mianzini,Hassan Mpwapwa alisema jitihada kubwa zinatakiwa kufanywa na walimu katika kuwafundisha wanafunzi kuhusu madhara ya rushwa.Kwani tatizo la rushwa linafahamika na hata shuleni linafahamika.

Alisema hakuna haja ya kuwa na somo maalumu la rushwa kwani masomo ni mengi sana.Bali walimu wajitahidi kuwafundisha wanafunzi wao.Akiweka wazi kwamba walimu wanazijua hata sheria zinazohusu TAKUKURU na madhara ya rushwa.

"Tatizo la rushwa linajulikana na hata shuleni tunalizungumzia.Ndio sababu baadhi ya wanafunzi wamejibu vizuri maswali yanayohusiana na rushwa.Sidhani kama kuna haja ya kuwa na somo maalumu.

Ziara ya maofisa hao wa TAKUKURU na Uhamiaji ilikuwa na lengo la kuhamasisha uanzishwaji wa klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi.

from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2BTcQKe

No comments