Breaking News

KILA MTU AWAJIBIKE BADALA KISINGIZIO CHA SIMBA INAPENDELEWA






NA SALEH ALLY
HATUWEZI kuwa na timu ambayo zinapendelewa halafu tukafanikiwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa. Kama tutakuwa na ligi yenye kiwango sahihi, basi tuna kila sababu ya kuwa na timu imara.


Kama Ligi Kuu Bara ina timu 20, tunaamini kumekuwa na ushindani mkubwa katika mechi nyingi hasa zile zinazoonyeshwa kwenye runinga ya Azam TV ambayo tunapaswa kuipongeza kwa kuleta mabadiliko makubwa kwenye mpira wa Tanzania baada ya mechi nyingi kuanza kurushwa moja kwa moja.


Umesikia watu wengi ambao ni wadau wa karibu kama wachezaji, makocha na kadhalika wamekuwa wakisema kuwa mechi nyingi zinazoonyeshwa moja kwa moja huwa hazina upendeleo.


Wanasema mechi nyingi zisizoonyeshwa, timu wenyeji wamekuwa wakipewa upendeleo wa wazi kuhakikisha wanabeba pointi za nyumbani maana yake si kwa uwezo wa mpira, jambo ambalo ni bayana linaudumaza mpira wa Tanzania ambao tunaupigania kukua.


Ili soka likue, lazima liwe na haki na nafasi kwa watu kuchezeshwa kwa haki, haki itawale na kutengeneza uimara unaotokana na ushindani sahihi kabisa.


Nimeamua kuandika makala haya baada ya kuona kuna kampeni ya chinichini ambayo haina faida kwa mpira wa Tanzania na inaonekana tumekuwa tunaoneana haya kwa kisingizio cha fulani shabiki wa timu fulani.


Kampeni za kusema Simba inapendelewa, Simba imekuwa ikipewa nafasi ya kushinda na kadhalika. Lakini wanaosema wamekuwa hawana uthibitisho wa zaidi ya asilimia 90 wa wanayoyasema.


Kinachoshangaza ni kuona na watu wengine ambao hawajaribu kutafakari yanayozungumzwa, wanayachukua na wao kuyazungumza kutoka kwa waliyoyasikia bila sababu au hoja sahihi.


Simba inapendelewa katika mechi ipi, kama imefunga mabao halali, vipi inapendelewa. Kuna bao ilipendelewa, jibu hapana, ila ilichezeshwa saa 8 badala ya saa 10 kama ilivyoelezwa. Kwani aliyecheza naye alicheza saa ngapi, naye alicheza muda huo pia. Sasa kupendelewa kunatokana na nini hasa?


Sote tunajua, Simba ndio wana timu bora kabisa katika Ligi Kuu Bara kwa msimu huu na hili linadhihirishwa na takwimu zao kwa maana ya wastani lakini hata hatua waliyofikia kimataifa na kuitangaza Simba mbali barani Afrika.


Pamoja na hivyo, unaona Simba iliyoifunga Al Ahly, AS Vita, JS Saoura na kutoka sare na TP Mazembe, imekwenda kufungwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar ambayo inapambana kuepuka kuteremka daraja katika Ligi Kuu Bara!


Hapo unaweza kujiuliza, kwamba kama ni hivyo, Simba inayopendelewa inafungwa vipi na Kagera Sugar, inahenyeshwa vipi na KMC lakini kabla ya hapo tuliiona ikipata shida kubwa dhidi ya Coastal Union pale Tanga.


Wanaofanya kampeni za kutengeneza lawama ni kampeni chafu na za kipuuzi, kampeni zinazoonyesha wameshindwa kufanya kazi zao na baada ya hapo wanasambaza maneno yatakayowalinda siku wakianza kuhojiwa kutokana na kufeli majukumu waliyokabidhiwa.


Kwa wale mnaosikia, vipi uamini vitu tofauti na ambavyo unaviona. Mtu hadi akuaminishe tofauti wakati na wewe uliona kabisa kila kitu kilivyo, vipi mtu mwingine akuaminishe tofauti na wewe uamini.


Wanaosambaza kile kisicho sahihi, vizuri kuwahoji kwa hoja badala ya kukubali kubeba wanachokisema hata kama ni pumba na kukisambaza pia.


Hatuwezi kuwa tayari kuona timu moja, mfano Simba inapendelewa halafu tukakaa kimya. Lakini kama si hivyo, basi mimi sitakaa kimya ili suala la mechi zinazochezwa tujadili mambo ya msingi na si haya ya kubabaisha kutokana na kuwapinga wanaobabaisha mambo.


Pia haitakuwa sahihi kuwasikia Simba sasa nao wakisema Yanga wanapendelewa baada ya ndani ya mechi tatu, kupoteza na kushinda moja wakati matarajio ilikuwa ni kushinda zote.


Tuache mpira uchezwe na kama kuna malalamiko yawe ya msingi badala ya kusambaza upuuzi.



from SALEH JEMBE

No comments