Mwenyekiti wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habibu Mchange akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakimshukuru Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa agizo la kuondolewa watu waliovamia kwenye bonde la Ihefu,
TEF na Mecira wametoa pongezi hizo leo Jumamosi, Desemba 24, 2022 ikiwa ni siku mbili zimepita tangu Rais Samia alipotoa kauli hiyo Desemba 22, 2022 wakati akizindua ujazaji maji Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere.
Bwawa hilo ambalo Juni 2024 litakamilika, litakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme.
Rais Samia alitaka utekelezaji wa haraka kufanyika kwa waharibifu wa mazingira hususan wanaozuia maji kupita katika mkondo wake kwa kujenga matuta na kuelekeza maji kwenda mashambani.
Mkuu huyo wa nchi alikuwa akiunga mkono maagizo ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyoyatoa Desemba 20, 2022 mkoani Iringa katika kongamano wa wadau wa mazingira lililoandaliwa na Mecira kwa kushirikiana na TEF.
Kabla ya Dk Mpango aliyekuwa mgeni rasmi kutoa maagizo hayo, Mecira na TEF walieleza kuna familia 12 za vigogo ambazo zimesababisha uharibifu wa mazingira ikiwemo kujenga matuta.
Ujenzi huo wa matuta umesababisha maji kupungua kwenye mito ya Ruaha Mkuu na Kilombero ambayo inachangia uzalishaji wa maji kwenye vyanzo vya umeme vya Kidatu na Mtera na kusababisha upungufu wa nishati hiyo.
Dk Mpango alisema “Serikali haitasita kuwachukulia hatua na hatutamwonea mtu. Uchunguzi ufanyike na wenye vibali wavilete ili kuviona, lengo ni kuboresha mazingira yetu.”
Leo Jumamosi Desemba 24, 2022, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile na Mwenyekiti wa Mecira, Habibu Mchange wamesema uamuzi Rais Samia ameonyesha ni mwanamazingira na ili nchi isonge inahitaji mazingira bora.
Babile amesema kongamano walilolifanya Iringa limekuwa na mafanikio makubwa, maelekezo aliyoyatoa Makamu wa Rais, Dk Mpango yameanza kutekelezwa.
“Lakini Rais Samia Suluhu Hassan naye ameongezea hilo na akasema hakuna aliyemkubwa katika nchi hii,” amesema Balile na kuongeza:
“Tunajua watu wengi wamewekeza kule kwenye mabonde, mashine, mitambo vya thamani kubwa kwa kuchukua mikopo benki, sisi tunapendekeza wapewe mwaka au miaka miwili ili kuwawezesha kuhamisha vifaa vyao.”
Amesema utaratibu wa kuwaondoa tusing'oe mazao yao, tuwape muda wa kuondoa mali zao. Amesema Bwawa la Nyerere halitaweza kujaa maji endapo mito inayotarajiwa kujaza ikiendelea kuharibiwa na wachache.
Naye Mchange amewapongeza waandishi na vyombo vya habari kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuungana kuonesha athari za uharibifu wa mazingira unaofanywa na watu mbalimbali.
“Tumeionesha nchi kuwa ulinzi wa mazingira na vyanzo vya maji si ya mtu bali ni ya kila mtu na sisi waandishi tumeonyesha hilo,” amesema Mchange
Pia, amempongeza Rais Samia akisema, “usikivu wake wa haraka, kutaka utekelezaji wa haraka wa maagizo ya makamu wa Rais umetufurahisha sana na sisi Mecira tutaendelea kushirikiana na mtu yoyote anayehitaji ushirikiano katika utunzaji wa mazingira.”
Amesema “mwezi mmoja uliopita kulikuwa na mgawo wa maji jijini Dar es Salaam, walioathirika ni wote, si CCM, Chadema au ACT-Wazalendo ni wote, kwa hiyo tushikamane kwa pamoja na vizazi vya leo na kesho bila woga au kumwogopa mtu.”
Kwa hisani ya Mwanachi Blog

