DP World yaleta mageuzi makubwa bandari ya Dar es Salaam
- Kipindi cha miezi mitano tangu ianze kuendesha gati 0-7, Serikali imeshakusanya bilioni 325.3
- Muda wa kuhudumia Meli za makasha gatini umepungua kutoka wastani wa siku saba hadi wastani wa siku tatu
- Gharama za matumizi ya uendeshaji wa bandari zimepungua hadi kufikia asilimia 2.7 ya makusanyo
Na Abraham Ntambara na Tunu Bashemela
SERIKALI imesema tangu Aprili 2024, Kampuni ya DP World
(Dubai) ilipoanza uendashaji wa shuguli za Bandari kwenye Bandari ya Dar es
Salaam kupitia Kampuni ya “DP World Dar es Salaam” mafanikio makubwa yameanza
kuonekana ndani ya kipindi hiki kifupi.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari
Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa
akizungumza na waandishi wa habari jiji kuhusu mafanikio ya uwekezaji wa DP
World katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akiainisha mafanikio hayo Msigwa alisema Mosi, ni kwamba kwa
mujibu wa mkataba uliosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP
World ni kuwa Kampuni hiyo inapaswa kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 250
sawa na shilingi bilioni 675 katika kipindi cha miaka mitano.
Hivyo Msigwa alibainisha kuwa katika kipindi cha miezi
mitano tayari wameshawekeza shilingi bilioni 214.425 sawa na asilimia bilioni
31 kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya kisasa, ukarabati wa mitambo iliyokuwa
ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na usanifu na usimikaji wa
mfumo wa TEHAMA wa kisasa wa uendeshaji wa Bandari.
Alieleza pili, ni kuwa wastani wa muda wa meli kusubiri umepungua kutoka siku 46 mwezi Mei 2024 hadi kufikia wastani wa siku saba (7) ikiwa ni siku 0 kwa meli za makasha, siku 12 kwa meli za kichele, na siku 10 kwa Meli za mizingo mchanganyiko.
Kwamba tatu, kutokana na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa (SSG na RTG) katika kupakia na kushusha mizigo, muda wa kuhudumia Meli za makasha gatini umepungua kutoka wastani wa siku saba (7) hadi wastani wa siku tatu (3) hivyo kupunguza idadi ya Meli zinazosubiri kutoka wastani wa meli 35 mwezi Septemba 2023 hadi wastani wa meli 15 mwezi Septemba 2024.
Nne, Msigwa alieleza kuwa katika kipindi cha miezi mitano
gharama za matumizi ya uendeshaji wa bandari zimepungua hadi kufikia asilimia
2.7 ya makusanyo wakati ambapo matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa asilimia 15.1
kwa mwezi kabla ya kukabidhiwa uendeshaji wa bandari kwa kampuni ya DP World
Dar es Salaam.
Alisema Tano, katika kipindi cha miezi mitano (Aprili hadi
Septemba 2024) tangu DPW Dar es Salaam waanze kuendesha Gati 0-7 katika Bandari
ya Dar es Salaam, Serikali imeshakusanya jumla ya shilingi bilioni 325.3 ikiwa
ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP
World, ikijumuisha tozo ya pango (land rent), tozo ya mrabaha (royalty), na
Ardhi (warfage).
Msigwa alieleza Sita kuwa, kutokana na kuongezeka kwa mapato
na kupungua kwa gharama za uendeshaji kufuatia maboresho yaliyofanyika,
serikali, kupitia TPA, imeanza uwekezaji katika miradi yenye thamani ya
shilingi trilioni 1.922 (USD 686.628 milioni) kwa kutumia makusanyanyo
yanayopatikana.
“Miradi hii ni Ujenzi wa Kituo cha Kupakulia Mafuta (SRT);
Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao (Mtwara), na Ujenzi wa Gati za Majahazi (Dhow
Wharf) Dar eS Salaam,” alisema Msigwa.
Aliongeza kueleza kuwa, Saba ni kuunganishwa kwa mifumo ya
forodha (Tanzania Customs Integrated System-TANCIS) na ile ya bandari (Tanzania
Electronic Single Window System-TeSWS). Hii imewezesha kupunguzwa/kuondolewa
kwa mifumo iliyokuwa inafanana na hivyo kupunguza muda wa kuondoa mizigo
bandarini, kuongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano.
Nane ni mapato ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
yameongezeka hadi kufikia shilingi Trilioni 1 mwezi Septemba 2024
ikilinganishwa na wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi Septemba 2023.
Kwamba hiyo imetokana na TRA kuweza kuchakata mizigo mingi zaidi ndani ya muda
mfupi.
Msemaji Mkuu huyo wa Serikali alibainishwa kuwa maboresho
yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam kufuatia kukabidhiwa kwa DP World
na makampuni mengine kuendesha Bandari ya Dar es Salaam yanaonesha kuwa na
faida kubwa kiuchumi kwa kuchochea kuongezeka kwa biashara na kuboresha
mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Kwamba uwekezaji huo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa
azima ya serikali ya kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango kuu la
usafirishaji mizigo katika ukanda wa Afrika.
Katika hatua nyingine akizungumzia kuhusu hali ya utendaji
wa Bandari nchini kwa kipindi cha miezi saba (Novemba, 2024 ikilinganishwa na
Mei hadi Novemba, 2023 Msigwa alisema, kwa kutambua kuwa bandari ni lango kuu
la uchumi kwa nchi yetu, Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa
kuimarisha miundombinu ya Bandari zetu za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na zile
zilizopo kwenye maziwa hali iliyochangia kuongeza ufanisi katika kuhudumia
shehena.
Alisema katika kipindi cha mwezi Mei 2024 hadi Novemba 2024,
kiwango cha shehena kilichohudumiwa na bandari zote zilizo chini ya TPA ni tani
milioni 16.5 ambayo ni ongezeko la asilimia 5.92 ya shehena ya tani milioni
15.6 iliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita (Mei 2023 hadi
Novemba 2023).
“Tumepata mafanikio makubwa pia kwa upande wa idadi ya
Makasha yaliyohudumiwa na bandari zote zilizo chini ya TPA katika kipindi cha
Mei 2024 hadi Novemba 2024 ambapop takwimu zinaonesha kuwa tumehudumia makasha
621,584 sawa na ongezeko la asimilia 3.29 ikilinganishwa na makasha 601,805
yaliyohudumiwa katika mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023),” alisema
Msigwa.


No comments