#KAZIINAONGEA
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewataka Wakemia binafsi na wa Serikali kuhakikisha wanazingatia miongozo, kanuni na sheria kwa kuongeza umakini wa matumizi sahihi ya kemikali ili kuepusha madhara kwa binadamu na mazingira.
Kikao hicho ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia, katika kuhakikisha matumizi sahihi ya kemikali yanazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuchukuwa tahadhari katika matumizi kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu Jingu ametoa kauli hiyo Disemba 11, 2024, Mkoani Dodoma, wakati akifungua kikao cha wadau wa kemikali nchini kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuwashirikisha zaidi ya Wataalamu 187 kutoka Makampuni na Taasisi mbalimbali ya nchini.
“Nitoe rai kwa sisi wote kuhakikisha tunatumia kemikali vizuri kwa matumizi sahihi na kwa ajili maendeleo ya makampuni yetu, nchi yetu, watu wetu na jamii zetu kwa ujumla na kuepusha madhara kwa watu na Mazingira kwa ujumla,” amesema Dkt. Jingu.
Amesema, maendeleo makubwa tunayoyapata kwenye sekta zote mchango wa Sekta ya kemikali ni mkubwa, kwahiyo matumizi sahihi ya kemikali ni kiungo muhimu.
Dkt. Jingu ameitaka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu na mafunzo kwa watendaji na wasafirishaji wa kemikali kuhusu matumizi sahihi ya kemikali kulingana na shughuli wanazozifanya bila kusahau matumizi ya vifaa kinga ili kujiepusha na vilema vya kudumu na athari zinazoepukika.
“Ofisi ya Mkemia iendelee zaidi kwa kufanya tathmini za mara kwa mara ya vifaa vya usalama katika maeneo yetu, itasaidia kuyaona maeneo ya shida na yenye ukakasi na kuendelea kuzingatiwa kanuni na miongozo,” amesema Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko awali akimkaribisha Katibu Mkuu amesema lengo la mafunzo hayo kwa wadau ni kuhakikisha wanakuwa na matumizi sahihi ya kemikali.
*#KAZIINAONGEA*

