TANZANIA KUZALISHA MEGAWATI 4,000 ZA UMEME IFIKAPO MWISHO WA MWAKA 2025
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba akifanya utambulisho katika mkutano wa Kimataifa wa Nishati unaowakutanisha Viongozi mbalimbali wa Afrika, Mashirika ya Kimataifa; Viongozi wa Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika na taasisi ya Rockefeller (M300) inayofanyika leo Januari 27, 2025 jijini Dar es salaam.
Tunu Bashemela na Abraham Ntambala
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto
Biteko amesema ifikapo mwisho wa mwaka 2025, uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme
utaongezeka hadi kufikia megawati 4,000.
Ameyasema hayo leo Januari 27, 2024 wakati akifungua
Mkutano wa Mawaziri wa Nishati, Viongozi wa Taasisi za Kimataifa za Kifedha,
Wataalam na Wadau wa Mashirika ya Kiraia, kuelekea Mkutano wa Nishati wa Wakuu
wa Nchi za Afrika utakaofanyika kesho jijini Dar es Salaam.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Tanzania inachukulia mkutano
wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika - Misheni 300 kama kichocheo cha
utekelezaji wa Sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati
endelevu, uhifadhi na ufanisi.
Ameeleza kuwa, pamoja na maendeleo ya nishati
tunayojivunia, bado nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati
kwani matarajio yake ni kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za
viwanda, madini na huduma za ukarimu jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa
kimkakati zaidi katika sekta ya nishati.
"Sera hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa
huduma za kisasa za nishati na kuongeza mchango wa nishati mbadala katika
mchanganyiko wa uzalishaji ili kuimarisha upatikanaji, uhakika na usalama wa
nishati," amesema Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa
mstari wa mbele katika kukuza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya
kupikia barani Afrika, jitihada ambazo zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na
kujumuishwa katika Azimio litakalotiwa saini katika mkutano huu, huku akitoa
wito wa ahadi na ushirikiano zaidi katika kuboresha upatikanaji wa suluhisho la
nishati safi ya kupikia barani mwetu.
Kwamba Tanzania inaimarisha muunganiko wa Afrika kwa
kuwa na miundombinu ya umeme inayounganisha nchi za Kenya, Burundi, Rwanda, na
Uganda, huku miundombinu ya kuunganisha Zambia ikiwa inaendelea.
Ametaja miongoni mwa mambo mengine yatakayofanyika
katika mkutano huo kuwa ni kushirikishana uzoefu; kupata ahadi muhimu za
kisiasa; kutumia ushirikiano ili kufungua uwekezaji wa sekta binafsi; kuanzisha
ushirikiano wa kufadhili miundombinu ya nishati; na kukubaliana mfumo wa
ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kiashiria cha Ufuatiliaji wa Maazimio
ili kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano
huo.
Ametoa rai kwa viongozi walioshiriki mkutano huo
kutumia fursa hiyo kuhitimisha Maazimio yanayoendana na matarajio ya bara la
Afrika ya nishati na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika kuyatekeleza.
"Ni matarajio yangu kwamba, mamlaka zinazohusika
za nishati katika kila nchi ya majaribio zitajitahidi kuhakikisha maazimio ya
nishati yanafanikishwa kupitia malengo na mipango ya hatua zinazolenga kuongeza
kiwango cha upatikanaji wa umeme, matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati
mbadala na mchango wa mtaji wa sekta binafsi katika kufanikisha upatikanaji wa
nishati", ameeleza Dkt. Biteko na kuongeza,
“Sasa ni wakati wa kufungua uwezo wa nishati wa bara
la Afrika na kukabiliana na pengo la nishati. Tuitumie fursa ya Mkutano huu
kuhitimisha Maazimio yanayoendana na matarajio yetu ya nishati na kuimarisha
ushirikiano unaohitajika kuyatekeleza,”.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay
Banga amesema kuwa Bara la Afrika linaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa
na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya
umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030.
“Tunaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa na
juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha Nishati ya
umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030,” amesema Banga.
Nae Rais wa Benki ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi
Adesina ameipongeza nchi ya Tanzania kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya
vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya
umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318.
“Tanzania imekua mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318,” amesema Dkt. Adesina.
Dkt. Adesina ametoa hakikisho kuwa lengo la
kuwafikishia umeme watu milioni 300 barani Afrika linakwenda kufanikiwa, ambapo
alieleza kuwa kunahitajika uwazi na uwajibikaji katika kufanikisha lengo hilo
ambapo alibainisha kwamba Mkutano huo unalengo la kuifungua Afrika kwenye eneo
la Nishati ya umeme, kuhakikisha wananchi katika Nchi za Afrika wanaunganishwa
na umeme.
Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Nishati,
Viongozi wa Taasisi za Kimataifa za Kifedha, Wataalam na Wadau wa Mashirika ya
Kiraia ambapo wamepata fursa ya kujadili na kukubaliana malengo, vipaumbele vya
sera, suluhisho, na ahadi za jinsi ya kutekeleza
Mpango wa Mission 300.
No comments