MUHIMBILI yatoa elimu ya ugonjwa wa Figo kwa wakuu wa shule na Polisi Dar

NA MWANDISHI WETU
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imetoa elimu kuhusu
ugonjwa ya figo na magonjwa yasiyoambukiza kwa walimu wakuu wa shule za
sekondari jijini Dar es Salaam pamoja na polisi kutoka Chuo cha Taaluma ya
Polisi (DPA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa
afya ya kiungo hicho.
Akizungumza kwenye hafla hiyo jana kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Faraja Chiwanga, ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Huduma za Tiba, alisema kuwa lengo kuu la kuadhimisha siku hii ni kuendelea
kuelimisha jamii kuhusu afya ya figo, ikiwa ni pamoja na njia bora za kujikinga
na magonjwa sugu ya figo ambayo yanatajwa kuwa tishio kwa jamii.
“Tunatumaini kuwa walimu hawa wataweza kufikisha elimu
hii kwa wanafunzi wao, hivyo kuwajengea msingi wa afya bora ya figo tangu
wakiwa vijana. Watakuwa mabalozi na wahamasishaji wakubwa wa afya ya figo
katika familia zao, jamii zao, na hata maeneo yao ya kazi.” alisema Dkt. Faraja
Naye Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH, Dkt. Jonathan
Mngumi, alieleza kuwa ugonjwa wa figo unawaathiri zaidi watu wenye umri wa
miaka 40-50, ambao ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya jamii na hii inaonesha
changamoto kubwa katika kupambana na ugonjwa huu, hasa kutokana na ongezeko la
mahitaji ya huduma za afya.
Nao Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Ralph Meela na Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule za Sekondari Dkt. Mavumba Hussein
waliushukuru uongozi wa MNH kuwapa elimu hiyo na kusema watakua mabalozi wazuri
sehemu zao za kazi na jamii inayowazunguka.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 7% ya watu nchini
Tanzania wanaugua ugonjwa sugu wa figo huku idadi ya wagonjwa wanaohitaji
huduma ya uchujaji wa damu ikitajwa kuongezeka kutoka 380 mwaka 2014/2016 hadi
2900 mwaka 2021/2022, na sasa wagonjwa wanaopatiwa huduma hiyo ni 3500.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “JE FIGO YAKO IKO SALAMA? Tutambue mapema, ilinde
afya ya figo yako”.
No comments