Breaking News

Operesheni ya DCEA na TANAPA yateketeza Ekari 614 za Bangi


Morogoro – Katika jitihada za kupambana na uhalifu wa dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wananchi wa maeneo ya jirani, wamefanikiwa kuteketeza mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 614 katika ushoroba wa hifadhi baina ya Mikumi na Nyerere.

Operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Julai 6 hadi 15, 2025, ilihusisha uvamizi wa maeneo yaliyotumiwa kinyume cha sheria kwa kilimo cha bangi, ambapo jumla ya kilogramu 3,741.9 za bangi kavu, pamoja na kilo 1,706 za mbegu za bangi, vilikamatwa. Zaidi ya hapo, kambi 72 za wakulima wa bangi zilibomolewa, huku watuhumiwa tisa (9) wakikamatwa kwa tuhuma za kuendesha shughuli hizo haramu.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alieleza kuwa mafanikio haya ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa kilimo na usambazaji wa bangi nchini. Alifafanua kuwa wahalifu sasa wamelazimika kusogea ndani zaidi ya maeneo ya hifadhi, jambo linaloonyesha athari ya moja kwa moja ya operesheni hizo.

> “Tunaona athari chanya. Idadi ya mashamba ya bangi inapungua na wakulima wanakimbilia maeneo ya mbali zaidi – ishara kuwa tumewakosesha fursa na mazingira salama ya kuendeleza uhalifu huu,” alisema Lyimo.

Aidha, DCEA imesisitiza kuendelea kushirikiana na vyombo vingine vya serikali, ikiwemo TANAPA na vikosi vya ulinzi na usalama, si tu katika kudhibiti maeneo haya ya hifadhi bali pia katika kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya bangi na kuwapa njia mbadala za kujipatia kipato halali.

Kwa upande wake, Kamanda Mkuu Msaidizi wa Kikosi cha TANAPA, Moses Oko Onyango, akimwakilisha Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, alisema kwamba walipokea taarifa za uwepo wa mashamba ya bangi katika eneo la Nyarutanga – mpakani mwa Mikumi na Nyerere – na wakaona ni lazima kuungana na DCEA ili kulinda hifadhi dhidi ya uvamizi wa kihalifu.

 “Hatutaruhusu hifadhi zetu zitumike kama maficho ya wahalifu. Ushirikiano wetu na DCEA ni wa kudumu katika kuhakikisha uhalifu huu unakomeshwa,” alisema Onyango.

Onyango aliongeza kuwa TANAPA iko tayari kutumia Kitengo chake cha Mahusiano na Jamii kueneza elimu kuhusu madhara ya bangi katika shule, vijiji na miji inayozunguka hifadhi. Pia aliahidi kuimarisha doria za pamoja ili kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanabaki salama dhidi ya kilimo haramu.

Mamlaka kwa mara nyingine imewaomba wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kupambana na biashara ya dawa za kulevya, kwa ajili ya usalama wa kizazi cha sasa na baadaye.

No comments