Zanzibar yadhamiria kuunga mkono mradi ya watu Wenye ulemavu,pia kuimarisha haki hao

 








Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali itaendelea kutoa mashirikiano ya karibu katika kuunga mkono miradi ya Watu Wenye Ulemavu ili kuhakikisha taifa linakuwa na jamii jumuishi yenye ustawi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa CADiR (Collective Action for Disability Rights), iliyofanyika katika Hoteli ya Madiinat Al-Bahr, Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mheshimiwa Othman alisema suala la haki na fursa kwa watu wenye ulemavu ni wajibu wa kitaifa unaohitaji mshikamano na mshirikiano wa pamoja.

Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa kundi hilo ikiwemo kuandaa sheria na sera maalum za kulinda haki zao, kuimarisha miundombinu rafiki, na kuanzisha mifuko ya kifedha. Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado mahitaji yao ni makubwa na mradi huo utasaidia kuongeza nguvu ya kuyafikia.

Akizungumzia tabia ya kuwatumia vibaya watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwaweka barabarani kuomba pesa, alisema changamoto hiyo inahitaji kushughulikiwa kisheria bila siasa na akawataka wote wanaohusika kubainishwa na kuchukuliwa hatua.

"Nataka kusema kwamba sheria na sera nzuri zipo, na pia mikataba ya kimataifa ipo wazi, lakini utekelezaji wake ndiyo changamoto; tunakwama wapi?" alihoji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Harusi Said Suleiman, alisema mradi huo ni faraja kubwa na unakuza juhudi za Serikali katika kujenga ustawi wa watu wenye ulemavu.

Naye Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alisema Wizara yake itaendelea kutoa kipaumbele cha huduma kwa watu wenye ulemavu, sambamba na kusisitiza ushauri wa kitabibu kwa familia ili kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na ulemavu. Aidha aliwataka wananchi na madereva kuepuka ajali zinazoongeza idadi ya walemavu nchini.

Mshauri Mkuu kutoka NAD (Norwegian Association for the Disabled), Bi Elise Bjastard, alipongeza kasi ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kulinda haki za watu wenye ulemavu na kueleza kuridhishwa kwa Norway kufadhili mradi huo.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia, asasi za kiraia, vikundi vya sanaa na watu wenye ulemavu, ambapo ulipambwa na burudani za watoto na ngoma ya Kibati.

Mradi wa CADiR ni wa miaka mitano, ukilenga kukuza na kuimarisha haki za watu wenye ulemavu Zanzibar na Tanzania Bara, kwa ufadhili wa Serikali ya Norway kupitia NAD.


Post a Comment

Previous Post Next Post