MSOMI WA SUDAN AWAPA ANGALIZO WATANZANIA WAOHUBIRI GHASIA
Na Mwandishi Wetu
Kauli ya "Tanzania si mahali pa majaribio ya ghasia" imesisitizwa kwa nguvu zote kufuatia barua ya wazi yenye uzito mkubwa kutoka kwa Profesa Hassan Mahmoud, msomi raia wa Sudan, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni Dubai kutokana na nchi yake kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Profesa Mahmoud, ambaye familia yake imepata hifadhi hapa nchini, anaiita Tanzania "kisiwa cha amani," lakini anatutahadharisha kuitunza amani hiyo kama "mboni ya jicho."
Profesa Mahmoud anaeleza kwa uchungu na maumivu jinsi taifa lake, ambalo lilikuwa tajiri na lenye matumaini makubwa, lilivyoteleza na kuzama katika dimbwi la vita lisilo na mwisho. Katika barua yake, anasimulia hali ya kutisha aliyoshuhudia ya majirani wakiuana, majiji yakigeuka magofu, familia zikisambaratika, na mamilioni ya watu wakilazimika kukimbia makwao—yeye akiwa mmoja wao.
Akielekeza ujumbe wake kwa Watanzania, Profesa Mahmoud anatoa onyo lenye hekima na maumivu: "Kilichotokea Sudan kinaweza pia kutokea kwenu endapo mtawaruhusu wanaohubiri vurugu kupata nafasi."
Anasisitiza kuwa, migogoro huanza na maneno, maneno ambayo yanaonekana madogo na yenye kusisimua katika mitandao ya kijamii, lakini huishia kwa vifo, umaskini, na uharibifu wa miaka mingi ya maendeleo.
Kitisho Kutoka 'Wanaharakati wa Ughaibuni'
Profesa Mahmoud anaitambua Tanzania kama nchi ya kipekee isiyo na migawanyiko ya kikabila, kidini, wala kiitikadi, na amani ya miongo mingi haipaswi kuchukuliwa kirahisi. Anahimiza kila Mtanzania kukataa kwa nguvu zote wale wanaotumia majukwaa ya siasa au mitandao ya kijamii kuhubiri chuki, fitina, na vurugu.
Jambo jingine la kutia wasiwasi ni kufichua kwake kuwa ana taarifa za kuaminika kwamba baadhi ya Watanzania walioko nje ya nchi "wanalipwa ili kutumia mitandao ya kijamii kueneza chuki na kuhamasisha migawanyiko ya kisiasa."
Msomi huyo ameonya kuwa yuko tayari kuwataja hadharani wale wote wanaonufaika na fedha hizo za uchochezi endapo wataendelea kuhatarisha amani ya nchi.
"Hawa 'wanaharakati wa ughaibuni' hawashambulii viongozi kwa mapenzi ya taifa, bali kwa maslahi yao binafsi," anasema, akitolea mfano wa maumivu yake ambapo familia yake ilikuwa miongoni mwa wachache walioweza kutoroka Sudan huku mamilioni wakiendelea kuteseka.
Si Siasa kwa Gharama ya Amani
Ni kweli kwamba kila taifa lina changamoto zake na Watanzania wanaweza kutamani haki, uwajibikaji, na uongozi bora. Hata hivyo, haya yote hayawezi kutafutwa kwa gharama ya amani.
Maneno ya Profesa Mahmoud yanatufanya tutafakari: Amani tuliyonayo haipaswi kuwa chombo cha majaribio ya kisiasa. Ni muhimu Watanzania tusikubali kurubuniwa na kelele za nje zisizoona machozi ya watoto wa Sudan au vilio vya kina mama waliosalia bila waume wao kwa sababu ya vita vilivyochochewa na maneno ya uchochezi kama yanayoenezwa sasa nchini Tanzania.
Huu ni wakati wa kutafakari kwa kina. Ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda misingi ya amani, kutunza urithi wetu wa utulivu, na kukataa siasa za vurugu na chuki. Tuchukue somo kutoka Sudan, tusisubiri kuona moshi kabla ya kugundua thamani ya utulivu tulionao leo. Tanzania inahitaji utulivu wake kuendeleza maendeleo, si majaribio ya ghasia za kisiasa.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/YoiJPVd

No comments