TMA YATANGAZA MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA NOVEMBA 2025 HADI APRILI 2026
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mwelekeo wa mvua za msimu wa Novemba 2025 hadi Aprili 2026 kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, ikidai kuwa msimu huo utatawaliwa na vipindi virefu vya ukavu pamoja na mtawanyiko wa mvua usioridhisha katika maeneo mengi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC), amesema mvua zinatarajiwa kuanza mwezi Novemba na kumalizika kati ya Aprili na Mei 2026, lakini hazitakuwa za kuridhisha katika maeneo mengi.
Maeneo yanayotarajiwa kuathirika ni pamoja na mikoa ya magharibi (Kigoma, Tabora, Katavi), kanda ya kati (Singida, Dodoma), nyanda za juu kusini magharibi (Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa), kusini (Ruvuma), ukanda wa pwani ya kusini (Lindi, Mtwara), pamoja na kusini mwa Morogoro.Amesema mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei 2026 katika maeneo mengi yanayopata mvua za msimu.
Dk. Chang'a amesema ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha nusu ya pili ya
msimu unaonza mwezi Februari mpaka Aprili, 2026 ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya mwezi Novemba, 2025 mpaka Januari, 2026.
Pamoja na mvua hizo kuwa za wastani hadi chini ya wastani, Dk. Chang'a ametoa angalizo uwepo wa matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani. Dk. Chang'a amewashauri wadau kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili waweze kujua mabadiliko yanayotokea katika mifumo ya hali ya hewa kwa kila siku.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/unD6hqV










No comments