KAMPUNI YA DMG YAKAMILISHA RIPOTI YAKINIFU UANZISHWAJI WA SAFARI FUPI ZA USAFIRI WA BAHARINI KWA TASHICO
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG) imetangaza kukamilika kwa utafiti yakinifu ambao utaisaidia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kuanza kutoa huduma za safari fupi kwa upande wa bahari nchini.
Tafiti hiyo yakinifu "Utoaji wa Huduma za Ushauri kwa Utafiti wa Uwezekano wa TASHICO kuingia katika usafirishaji wa baharini wa safari fupi katika Bahari ya Hindi" iliwaleta pamoja wadau muhimu ili kujadili matokeo ya kina ya utafiti huo ambao umechunguza fursa za kimkakati za Kampuni ya TASHICO kupanuka zaidi kutoka kutoa huduma za usafirishaji kwenye maziwa makuu hadi usafirishaji wa safari fupi baharini.
Mpango huu wa kuanza kwa safari za baharini unafanywa na Kampuni ya TASHICO unakuja ukiwa na malengo mapana ya kukuza biashara na mahusiano katika eneo la Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi kwa ujumla.
Utafiti huo ulifanywa kwa kukusanya taarifa kutoka zaidi ya mamlaka tisa katika nchi za Kenya, Comoros, Mauritius, Seychelles, Madagaska na Réunion.
Utafiti huo unatoa majibu kwa maswali manne muhimu ambapo tafiti inabainisha aina za mizigo ambayo inaweza kusafirishwa kwa njia ya bahari.
Utafiti huo unaonyesha vile vile njia za usafirishaji baharini zinazofaa kiuchumi na kupendekeza aina za meli, ukubwa na vipimo vinavyofaa.
Vile vile utafiti huo unaelezea muundo wa gharama ikijumuisha mtaji na uendeshaji.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na Bw. Maseke Mabiki, Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Uchukuzi pamoja naye alikuwepo Mhandisi Shomari Shomari, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafiri katika Wizara ya Uchukuzi aliemwakilisha Katibu Mkuu na kutoa hotuba kwa niaba ya uongozi wa wizara.
Warsha hiyo ilishuhudia ushiriki wa wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi, ikijumuisha wawakilishi kutoka Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Fedha, Mamlaka mbalimbali kama TASAC, LATRA, TPA, TCAA, EWURA, Chuo cha Bahari, TASAA, TSC, Taasisi za Kibenki kama CRDB na NMB, Kituo cha Mahusiano ya ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, wadau mbali mbali waliipongeza Kampuni ya DMG Kwa kutayarisha taarifa ya kitaalamu na bobevu iliyosheheni mambo muhimu kwa uanzishwaji wa safari fupi za baharini zitakazofanywa na Kampuni ya TASHICO.
"Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Wizara ya Uchukuzi, Uongozi wa TASHICO na wadau wote walioshiriki katika kufanikisha na kutayarisha taarifa hii ya kitaalamu ambayo ina lengo zuri la uanzishwaji wa safari fupi za baharini na Kampuni ya TASHICO," Mkurugenzi Mkuu wa DMG, Rayton Kwembe", alisema.












from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/W75osF4










No comments