Breaking News

WAZIRI NDEJEMBI AITAKA PURA KUWAJENGEA UWEZO WATANZANIA KUSHIRIKI MRADI WA LNG

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratous Ndejembi, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuimarisha mipango yake katika ukusanyaji wa data sahihi, tathmini ya vitalu vya utafiti, na maandalizi ya Watanzania kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika (LNG).

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo wakati wa Kikao cha Tano cha Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi la PURA kilichofanyika mkoani Morogoro leo Februari 26, 2026.

 Amesisitiza kwamba sekta ya nishati ina nafasi ya kipekee katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo PURA inatakiwa kuhakikisha mipango yake inaendana na maono hayo.

“Sekta ya Nishati imetambuliwa kama moja ya vichocheo muhimu vya uchumi wa taifa. Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati zina wajibu mkubwa kuhakikisha upatikanaji endelevu, salama na wa uhakika wa rasilimali za mafuta na gesi asilia,” amesema Mhe. Ndejembi.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka PURA kuongeza juhudi katika ukusanyaji na usimamizi wa data za kijiolojia na kufanya tafiti za awali, hasa ikizingatiwa kwamba maeneo makubwa ya nchi bado hayajafanyiwa utafiti wa kina.

“Takwimu sahihi ni msingi wa kuvutia uwekezaji na kuongeza ugunduzi wa rasilimali. Hatuwezi kuendeleza sekta bila taarifa za kutosha na tafiti madhubuti,” amesisitiza.

Waziri huyo pia ameagiza PURA kufanya tathmini ya kina katika vitalu vilivyopo, hususan katika ukanda wa Tanga, Ruvu, na maeneo mengine, ili kubaini iwapo wamiliki wa vitalu wanafanya shughuli za utafutaji kama inavyotakiwa.

 Ameongeza kuwa si vyema kwa vitalu kukaa mikononi mwa wawekezaji wasioendeleza shughuli za utafutaji, na mamlaka za udhibiti zinapaswa kuchukua hatua pale inapobainika hakuna maendeleo yanayofanyika kwa manufaa ya Taifa.

Akizungumzia mradi wa LNG, Mhe. Ndejembi amewataka PURA kuanza mapema kuandaa mkakati wa kujenga uwezo wa kitaasisi katika kusimamia mradi huo. 

Sambamba na hilo, amewahimiza kuandaa Watanzania kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa LNG, badala ya kusubiri utekelezaji wa mradi kuanza.

Awali katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amewataka PURA kusimamia majukumu yake ya msingi kama yanavyoainishwa katika malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

         

No comments