ARUSHA DC YATENGA JUMATANO KUSIKILIZA KERO, WANAWAKE WAHIMIZWA KUMILIKI ARDHI KIHALALI
Na Bora Mustafa, Arusha.
Uongozi wa Wilaya ya Arusha umetangaza kuanzisha rasmi siku maalum ya kushughulikia kero za wananchi katika ngazi ya kata na mitaa, hatua inayolenga kupunguza mlundikano wa malalamiko katika ofisi za wilaya.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Machi 03,2026 , Mkuu wa Wilaya ya Arusha,mhe. Joseph Mkude, amesema kuwa kuanzia sasa kila siku ya Jumatano wananchi watapata fursa ya kuwasilisha na kusikilizwa kero zao katika maeneo yao.
Amesema utaratibu huo utasaidia kupunguza idadi ya wananchi wanaolazimika kufika ofisi za wilaya kufuatilia malalamiko yao, pamoja na kutoa nafasi kwa uongozi kushughulikia masuala mengine ya maendeleo.
Pia amesema kuwa lengo ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili wapate majibu kwa wakati.
Pamoja na hilo, Mkude amesema kuwa kila Ijumaa katika ngazi ya kata kutakuwa na ufuatiliaji wa kero zilizowasilishwa ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi.
Pia amesema kuwa Jumatano ya mwisho wa mwezi itatengwa kwa ajili ya kusikiliza kero katika viwanja vya wilaya, hatua itakayowapa nafasi wananchi wengi zaidi kuwasilisha changamoto zao.
Katika hatua nyingine, amesema kuwa kliniki maalum ya ardhi inaendelea kufanyika wilayani humo kwa lengo la kutoa elimu na kurahisisha taratibu za umiliki wa ardhi, hususan kwa wanawake. Amesema mwanamke ana haki ya kisheria ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa mtu mwingine yeyote, pamoja na kwamba jamii bado inahitaji kupewa elimu zaidi kuhusu haki hiyo.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa inayochangia migogoro ya ardhi ni ukosefu wa uelewa wa taratibu sahihi za ununuzi na umiliki wa ardhi. Amesema wanasheria wa wilaya pamoja na maafisa ardhi wameelekezwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu ya kutosha kuhusu sheria na taratibu hizo.
Aidha, amesema wananchi wote wenye uhitaji wa kupimiwa maeneo yao wanatakiwa kufika katika ofisi za ardhi ili kupatiwa huduma za upimaji pamoja na kuandaliwa nyaraka muhimu za umiliki.
Pia amewahimiza kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ili kuepuka migogoro ya baadaye na kumiliki ardhi kihalali.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/Km9s28G
No comments