Breaking News

MAANDALIZI SIKU YA UHURU WA VYOMBO HABARI YAIVA, WADAU 600 KUKUTANA ARUSHA APRILI 28

Maandalizi ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (World Press Freedom Day 2026) nchini Tanzania yamepamba moto, huku Waziri Mkuu, Mhe. Lameck Mwigulu Nchemba, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo kitakachofanyika Aprili 30, jijini Arusha.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaratibiwa na Wizara ya Habari kupitia Idara ya Habari-MAELEZO, kwa kushirikiana na Shirika la UNESCO na Taasisi ya Tech & Media Convergency (TMC). Chini ya kauli mbiu inayohimiza uhuru wa vyombo vya habari kwa ajili ya haki za binadamu na usalama, wadau zaidi ya 600 wanatarajiwa kukutana kutathmini hali ya tasnia nchini.

                                Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari-MAELEZO Evody Kyando

Bi. Asha D. Abinallah Mkurugenzi wa TMC naMwenyekiti wa kamati ya maandalizi kwa mwaka 2026 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam

Nancy Angulo mwakilishi kutoka UNESCO

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi na Mkurugenzi wa TMC, Bi. Asha D. Abinallah, amesema maadhimisho hayo yataanza Aprili 28 na kuhitimishwa Mei 1. Amesema mwaka huu, kipaumbele kikubwa kitatolewa kwenye hali ya kiuchumi ya vyombo vya habari, hususan mzigo wa madeni yanayokabili vyombo vya habari nyingi habari nchini.

"Tutajadili mustakabali wa ukuaji wa vyombo vya habari, tukihusisha watunga sera, wamiliki, waandishi, na watetezi wa haki za kidijitali. Lengo ni kuona jinsi gani tunavyoweza kuimarisha uchumi wa tasnia hii ili iendelee kutoa mchango wake kwa Taifa," alisema Bi. Asha.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari-MAELEZO, Evody Kyando, amesisitiza kuwa serikali inatambua umuhimu wa uhuru wa habari lakini akatoa wito kwa wanahabari kuzingatia weledi. "Tunawahimiza waandishi kutekeleza majukumu yao kwa uhuru, lakini uhuru huo uambatane na uwajibikaji na maadili ya kazi," alisema Kyando.

Maadhimisho hayo yatapambwa na mfululizo wa matukio ikiwemo mbio za hiari (Fun Run) mkoani Arusha, maonyesho ya ubunifu wa kidijitali, pamoja na mijadala ya kisera inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa waandishi na watayarishaji wa maudhui (content creators).

Nancy Angulo kutoka UNESCO amethibitisha kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha uhuru wa habari, huku akibainisha kuwa jukwaa la Arusha litakuwa fursa muhimu ya kujadili usalama wa waandishi na usawa wa kijinsia ndani ya vyumba vya habari.

No comments