Breaking News

KUTOKA NDOTO HADI FURAHA: UMEME KUMFIKIA BIBI SESILIA

 



Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, alipata nafasi ya kusikiliza ombi la Bibi Sesilia Charles wakati wa mazungumzo na wananchi katika Kitongoji cha Elimu, Kijiji cha Mushinde, Kata ya Buwangongo wilayani Geita. Bibi Sesilia alimueleza kuwa licha ya umeme kufikishwa katika kitongoji chao, bado nyumba yake haijaunganishiwa huduma hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Bibi Sesilia alimuelekeza Naibu Waziri kwa kidole akionyesha ilipo nyumba yake, akieleza kuwa nguzo ya umeme tayari imesimamishwa karibu na eneo hilo na kuomba kusaidiwa ili naye aweze kuunganishiwa umeme. Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri alisema, “Pole sana Bibi, ombi hili nalifanyia kazi hapa hapa.”

Bila kupoteza muda, Naibu Waziri alimuita Mhandisi wa REA na kumuelekeza kwenda pamoja na Bibi Sesilia nyumbani kwake ili kumsaidia kufanya taratibu za maombi ya kuunganishiwa umeme na kuhakikisha anaunganishiwa haraka iwezekanavyo.

Akitekeleza maelekezo hayo, Mhandisi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) aliahidi kuchukua hatua mara moja na kuhakikisha Bibi Sesilia anapata huduma hiyo muhimu.

Baada ya kupata matumaini ya kuunganishiwa umeme, Bibi Sesilia alionekana mwenye furaha kubwa akicheza kwa shangwe na kusema, “Mama Samia oyeee! Sasa na mimi naletewa umeme mpaka ndani.”

Tukio hilo lilitokea tarehe 14 Machi 2026 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipozindua mradi wa upelekaji umeme katika vitongoji 15 kwa kila jimbo la uchaguzi (HEP 2A) kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kitongoji hicho.

No comments