Breaking News

SALOME AHIMIZA WADAU KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NCHINI



Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ametoa wito kwa wadau na waandaaji wa majukwaa mbalimbali ya wanawake nchini kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na kutoa elimu itakayosaidia kuwaokoa wanawake dhidi ya changamoto zitokanazo na matumizi ya nishati isiyo safi.

Salome Makamba ameyasema hayo leo, tarehe 25 Machi 2026, katika hafla ya maadhimisho ya miaka 10 ya Malkia wa Nguvu Legacy Mark 2026 iliyoandaliwa na Clouds Media Group, inayofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Ameitaka pia Jukwaa la Malkia wa Nguvu kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mhamasishaji namba moja barani Afrika wa ajenda hiyo.

“Malkia wa Nguvu Levels isimuache Mwanamke wa Kitanzania akaendelea kuteketea kwa kutumia Nishati isiyo safi. Wizara ya Nishati tunacho kipaumbele cha kuhakikisha kufikia mwaka 2030 Watanzania zaidi ya asilimia 80 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia” amesema Salome Makamba.

Aidha, Salome ameeleza kuwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali zinahitaji kuungwa mkono na majukwaa mengine kama Malkia wa Nguvu, ambayo yana nafasi muhimu ya kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuweka kipaumbele katika utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi.

Amesisitiza kuwa nishati safi inaleta mapinduzi makubwa katika maisha ya mwanamke kwa kuondoa madhara yatokanayo na moshi wa kuni na mkaa, kufungua fursa za biashara, kuongeza kipato, pamoja na kupunguza hatari na unyanyasaji unaoweza kujitokeza wakati wa kutafuta nishati katika maeneo hatarishi.

“Tukiamua kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha hakuna mwanamke anayebaki nyuma kimaendeleo. Tushirikiane na kuwezeshana ili siku moja tujivunie jitihada hizi za kumkomboa mwanamke na kuona matunda yake yakinufaisha jamii nzima,” amesisitiza Makamba.

Vilevile, Salome ameipongeza Clouds Media Group kwa mafanikio ya miaka 10 ya Jukwaa la Malkia wa Nguvu, ambalo limeendelea kuwawezesha wanawake kupiga hatua kimaendeleo kupitia fursa mbalimbali, kuimarisha mitazamo yao, na kuwafungulia milango ya kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Malkia wa Nguvu, Liliane Masuka, amesema jukwaa hilo ni chombo muhimu cha kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kutambua na kuthamini juhudi zao katika sekta mbalimbali, huku likiadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.

No comments