Breaking News

SHUWASA YAKUTANA NA WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA, YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI



Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imekutana na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Shinyanga kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi.

Kikao hicho cha kazi kimefanyika leo Jumamosi Machi 14, 2026 mjini Shinyanga na kuongozwa na Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Katopola amesema SHUWASA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za maji kwa wananchi wa Shinyanga, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya maji, kupanua mtandao wa usambazaji na kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya SHUWASA na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu huduma za maji, miradi inayoendelea pamoja na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Aidha amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya maji, kulinda miundombinu ya maji pamoja na kusaidia kufikisha maoni na changamoto za wananchi ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.

Kwa upande wao, waandishi wa habari wameeleza utayari wa kuendelea kushirikiana na SHUWASA katika kuhabarisha umma kuhusu masuala ya maji, wakisema kuwa taarifa sahihi na kwa wakati zitasaidia kuongeza uelewa wa wananchi na kuchochea maboresho ya huduma kwa jamii.




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/wG5otNC

No comments