DODOMA YAPOKEA BILIONI 43 KUSAMBAZA UMEME KATIKA VITONGOJI 379





Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mkoa wa Dodoma umepokea shilingi bilioni 43 kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya kupeleka huduma ya umeme katika vitongoji 379, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya nishati ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema fedha hizo zimekuja baada ya Mkoa kukamilisha mpango wa usambazaji umeme katika vijiji 564, huku Serikali sasa ikielekeza nguvu zake kwenye kufikisha huduma hiyo katika vitongoji vilivyobaki.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichowakutanisha viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi jijini Dodoma, Senyamule alisema upatikanaji wa fedha hizo unaonesha dhamira ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa nishati ya uhakika.

“Ilani iliyopita ilielekeza umeme kufika katika kila kijiji, na hatua hiyo imefikiwa. Sasa Ilani ya sasa inalenga kuhakikisha kila kitongoji kinapata umeme ifikapo mwaka 2030, na tayari tumepata shilingi bilioni 43 za kuanza utekelezaji wa kazi hiyo,” alisema Senyamule.

Alibainisha kuwa Tanzania imeendelea kuwa kinara wa usambazaji wa umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, mafanikio ambayo yamechangia Rais Samia kupata tuzo mbalimbali za kutambua mchango wake katika sekta ya nishati.

Mbali na mradi huo wa kusambaza umeme vijijini na vitongojini, Senyamule alisema Mkoa wa Dodoma una nafasi muhimu katika mfumo wa usafirishaji wa umeme nchini kupitia ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Kupoza Umeme cha Zuzu kinachoendelea kujengwa jijini humo.

Alieleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu na utakuwa kiungo muhimu cha kupokea umeme unaozalishwa katika Bwawa la Mwalimu Nyerere kabla ya kusafirishwa kwenda katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

“Kituo cha Zuzu kitakuwa miongoni mwa miundombinu muhimu ya nishati nchini. Umeme utakaotoka Bwawa la Mwalimu Nyerere utapitia hapa kwa ajili ya kupozwa na kisha kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi,” alisema.

Kikao hicho kilihusisha viongozi wa makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, bodaboda, bajaji, mama na baba lishe, wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati, vikundi vya wanawake, vijana na wadau wengine wa maendeleo, kwa lengo la kuwapa taarifa kuhusu mafanikio ya Mkoa na fursa zinazotokana na miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.

Utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 379 unatarajiwa kuongeza shughuli za uzalishaji, biashara na huduma za kijamii katika maeneo mengi ya Mkoa wa Dodoma, huku ukiwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa wananchi na maendeleo ya Mkoa kwa ujumla..








from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/oMOX4If

Post a Comment

Previous Post Next Post