
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewaomba na radhi na kuwapa pole wateja wa shirika hilo kufuatia hitilafu ya umeme iliyotokea jana jioni na kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza leo Julai 28, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Lazaro Twange amesema hitilafu hiyo ilianza majira ya saa moja jioni baada ya kutokea tatizo katika Gridi ya Taifa, lakini wataalamu wa TANESCO walifanikiwa kurejesha huduma usiku huohuo.
Alisema kwa sasa umeme umeimarika na wateja wote nchini, ikiwemo Zanzibar nao wanaendelea kupata huduma kama kawaida.
“Gridi ya Taifa ni mfumo unaounganisha vituo vya kuzalisha umeme,njia za kusafirisha umeme na vituo vya kupunguza au kuongeza msukumo wa umeme kabla ya kuwafikia wateja.

Amesema hitilafu ya jana ilisababishwa na matatizo yaliyotokea kwa wakati mmoja katika njia tatu za kusafirisha umeme pamoja na kituo kimoja cha gridi, hali iliyosababisha mfumo mzima kujizima kwa ajili ya kujilinda dhidi ya uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Amesema wataalamu wa TANESCO waliendelea kufanya kazi usiku kucha kurejesha huduma na kwa sasa wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha hitilafu hiyo na kuweka hatua za kuzuia isitokee mara kwa mara.
Mkurugenzi huyo pia aliwapa pole wateja wote walioathirika, wakiwemo wasafiri wa treni ya umeme ya SGR, Hospitali ya Benjamin Mkapa, wafanyabiashara, wajasiriamali pamoja na wananchi waliokosa huduma mbalimbali kutokana na kukatika kwa umeme.
Twange ameahidi kuwa TANESCO itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha Gridi ya Taifa na kuhakikisha huduma ya umeme inakuwa ya uhakika zaidi nchini.

