📍Dodoma
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeeleza kuwa inaongeza kasi ya kufanya tafiti za jiosayansi nchini ili kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa GST, Mha. Ally Samaje, amesema taasisi hiyo ndiyo msingi wa mnyororo mzima wa sekta ya madini kwa kuwa hukusanya, kuchakata, kuhifadhi na kusambaza taarifa muhimu za jiosayansi kwa wawekezaji na wadau wengine.
Amesema hadi sasa GST imekamilisha utafiti wa jiolojia kwa asilimia 98 ya eneo lote la Tanzania, huku utafiti wa jiofizikia wa skeli ndogo (low resolution airborne geophysical survey) ukifikia asilimia 100. Hatua hiyo imeendelea kuwapa wawekezaji taarifa za awali zinazowawezesha kutambua maeneo yenye fursa za madini na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji.
Kwa upande wa utafiti wa jiofizikia wa kina (High Resolution Airborne Geophysical Survey), Mha. Samaje amesema umefikia asilimia 16 ya eneo la nchi. Hata hivyo, maandalizi ya kuongeza kiwango hicho yanaendelea kupitia programu mpya ya urushaji ndege katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya programu hiyo itahusisha utafiti katika eneo linalokadiriwa kuwa asilimia 18 ya ukubwa wa Tanzania, hatua itakayoongeza kiwango cha utafiti huo hadi asilimia 34 baada ya kukamilika. Amesema mkandarasi wa kutekeleza kazi hiyo tayari amepatikana.
Aidha, amesema awamu inayofuata itafanyika katika eneo la katikati ya Tanzania lenye ukubwa wa takribani asilimia 19 ya nchi, jambo litakalowezesha kufikia zaidi ya asilimia 50 ya utafiti wa kina wa jiofizikia, lengo ambalo Serikali imejiwekea kulifikia kabla ya mwaka 2030.
Akizungumzia utafiti wa jiokemia, Mha. Samaje amesema GST imefikia asilimia 24 ya eneo la nchi, na katika mwaka huu wa fedha taasisi itafanya tafiti katika maeneo mapya 18 ili kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 30.
Ameeleza kuwa maeneo mengi yatakayofanyiwa utafiti yamechaguliwa kutokana na uwepo wa wachimbaji wadogo, ambapo taarifa zitakazopatikana zitawawezesha kufanya uchimbaji kwa uhakika badala ya kubahatisha, kuongeza uzalishaji, kuboresha kipato na kupunguza hasara za kuwekeza bila kuwa na taarifa za jiosayansi.
Kwa mujibu wa Mha. Samaje, taarifa hizo pia zitawasaidia wachimbaji wadogo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha, huku GST ikiwa tayari imethibitisha matokeo ya tafiti zake ili kuongeza imani ya taasisi hizo kwa wachimbaji.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa programu hizo unawezeshwa na Mfuko wa Utafiti wa Madini unaofadhiliwa na Serikali kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya Sekta ya Madini kwa ajili ya kuzielekeza kwenye kufanya tafiti za madini nchini.
"Nichukue fursa hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuanzishwa kwa mfuko huo ambao utawezesha kuongeza kasi ya kufanya tafiti za madini nchini" ameongeza Mha. Samaje.
Amesisitiza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiosayansi utapunguza hatari kwa wawekezaji, kuongeza uwekezaji katika utafiti na uchimbaji wa madini, kuchochea uanzishaji wa migodi mipya, kuimarisha viwanda vinavyotumia madini kama malighafi na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa, hatua itakayosaidia kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
