RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia
kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) Agosti,22 2026 katika eneo la mradi Rufiji, Mkoa wa Pwani.

JNHPP ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati katika historia ya sekta ya nishati nchini.Kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 za umeme.
Akizungumza leo Agosti, 15 2026 jijini Dar es Salaam Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema hatua inayotarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Taifa wa kuzalisha na kusambaza umeme wa uhakika.
“Mradi huu umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.Ujenzi wa mradi ulianza Juni 2019 na kukamilika Machi 2025, ukiwa umeajiri takribani wafanyakazi 12,000 wakati wa ujenzi,”amesema.
Ameeleza kuwa kwa sasa, uwezo wa mitambo yote ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani Megawati 4,646, huku JNHPP pekee ikichangia Megawati 2,115.
Ndejembi amesema tangu kuanza kuzalisha umeme, kituo hicho kimeendelea kuongeza kiwango cha umeme kinachoingia katika Gridi ya Taifa.
Hatua hiyo imechangia kupunguza changamoto ya upungufu wa umeme iliyokuwa ikisababisha mgao katika maeneo mbalimbali nchini.

“Takwimu zinaonesha kuwa hadi Mei 31, 2026, JNHPP ilikuwa imezalisha takribani asilimia 44.9 ya jumla ya umeme uliozalishwa na kuingia katika Gridi ya Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja,”amesema.
Aidha amesema bwawa la JNHPP lina uwezo wa kuhifadhi takribani mita za ujazo bilioni 33 za maji, kiasi kinachokadiriwa kuwa mara 10 ya uwezo wa Bwawa la Mtera.Mbali na kuzalisha umeme, mradi huo unatarajiwa kuwa na manufaa katika sekta za kilimo cha umwagiliaji, utalii na matumizi ya maji kwa binadamu.
Amesema uwepo wa umeme wa uhakika utasaidia kuongeza uzalishaji viwandani, kukuza biashara na kuweka mazingira bora kwa uwekezaji.
JNHPP pia unatajwa kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hasa katika kuimarisha miundombinu ya nishati na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, uzinduzi huo utakuwa tukio la kihistoria katika safari ya Tanzania ya kujenga mfumo wa nishati wenye uhakika na uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi.
