Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumamosi Agosti 22, 2026, amezindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), kilichopo Rufiji, Mkoa wa Pwani.
JNHPP ni mradi mkubwa wa kimkakati katika sekta ya nishati nchini, wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 kupitia mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa Megawati 235.
Mradi huo umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452, fedha za ndani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ujenzi wake ulianza Juni 2019 na kukamilika Machi 2025.
Uzinduzi huo unaashiria hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza uzalishaji, kuchochea uwekezaji na kuimarisha ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, hadi Mei 31, 2026, JNHPP ilikuwa imechangia nusu ya umeme wote unaozalishwa na kuingizwa katika Gridi ya Taifa.
Mradi huo pia unatajwa kuwa na mchango katika kuimarisha usalama wa nishati nchini na kupunguza changamoto za upungufu wa umeme zilizokuwa zikisababisha mgao katika vipindi vya nyuma.
Pamoja na kwamba kituo hicho kunatumia teknolojia ya hali ya juu, lakini habari njema ni kwamba kinaendeshwa na Watanzania kwa asilimia 100.




