Na Dotto Kwilasa,DODOMA
Tanzania imeokoa zaidi ya tani milioni 1.4 za mazao ya nafaka ambazo zingepotea kutokana na mashambulizi ya visumbufu, baada ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kudhibiti kwelea kwelea milioni 233.5 pamoja na viwavi jeshi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Agost 27,2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph C. Ndunguru, amesema hatua hizo ni sehemu ya mafanikio ya Mamlaka katika mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo Tanzania ilifikia kiwango cha utoshelevu wa chakula cha asilimia 130, huku uzalishaji ukifikia tani 23,783,128.
Prof. Ndunguru amesema kwelea kwelea hao walivamia wilaya 21 na kudhibitiwa kwa njia ya anga kwa kutumia ndege na ndege nyuki, hatua iliyosaidia kuokoa takribani tani 1,092,780 za nafaka zikiwemo mtama, uwele na mpunga.
Kwa upande wa viwavi jeshi, amesema TPHPA ilifanya udhibiti katika halmashauri 52 zilizoathirika, ambapo jumla ya lita 54,846 za viuatilifu zilitumika katika mashamba yenye ukubwa wa ekari 228,525, na kuokoa takribani tani 342,787.5 za nafaka.
Mbali na udhibiti wa visumbufu, TPHPA imeendelea kutumia teknolojia za kisasa katika kutambua magonjwa na visumbufu vya mimea. Katika Mpwapwa, kwa mfano, uchunguzi wa kutumia PCR na DNA Sequencing ulibaini kuwa nzige waliodhaniwa kuwa nzige wekundu walikuwa aina ya Tree Locust – Anacridium incisum, huku uchambuzi wa BLAST ukionesha ufanano wa asilimia 96.52.
MASOKO YA NJE YAFUNGUKA
Prof. Ndunguru amesema TPHPA imeendelea kuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha mazao ya Tanzania yanakidhi viwango vya afya ya mimea vinavyohitajika na nchi wanunuzi.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, kampuni nane mpya za Tanzania ziliruhusiwa kusafirisha parachichi kwenda China, na kuongeza jumla ya kampuni zilizoruhusiwa kufanya biashara hiyo hadi 24.
Aidha, kampuni 444 za Tanzania zimesajiliwa katika mfumo wa forodha wa China (GACC) kwa ajili ya kusafirisha mazao mbalimbali, huku kampuni tano za ufukiziaji zikiwa zimesajiliwa kwa ajili ya huduma zinazohitajika kwenye mazao yanayopelekwa nchini humo.
Tanzania pia imefungua soko la Seychelles kwa mazao 10, yakiwemo kabichi, parachichi aina ya Hass, maharage mabichi, karoti, viazi, kitunguu saumu, tangawizi, kitunguu maji, nanasi na mimea ya viungo.
Masoko mengine yaliyofunguliwa au kuwezeshwa ni pamoja na parachichi kwenda Afrika Kusini, India na China; soya kwenda China; mashudu ya pamba na alizeti kwenda China; mahindi ya njano kwenda Misri; ndizi mbichi kwenda Afrika Kusini, pamoja na mazao mbalimbali kwenda Seychelles.
VIUATILIFU 205 VIONDOLEWA SOKONI
Katika kulinda afya ya wakulima, walaji na mazingira, TPHPA imeimarisha udhibiti wa viuatilifu. Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, Mamlaka ilikagua maduka 5,157, kutoa vibali 3,831 vya kuingiza viuatilifu nchini na kusajili viuatilifu vipya 508.
Jumla ya sampuli 3,463 zilichukuliwa na kuchambuliwa maabara, ambapo sampuli 132, sawa na asilimia nne, hazikukidhi viwango na wahusika waliagizwa kurejesha shehena hizo.
Aidha, Januari 2026, TPHPA iliondoa sokoni viuatilifu 205 vilivyobainika kuwa na viambata amilifu hatarishi, huku viuatilifu 675 vikiondolewa kwenye orodha ya vilivyosajiliwa kutokana na kutohuishwa usajili kwa zaidi ya miaka 10.
TSH BILIONI 2.8 ZATUMIKA KUBORESHA MAABARA
Katika kuongeza uwezo wa uchunguzi, TPHPA imenunua mashine tano za kisasa za maabara zenye thamani ya Sh2.8 bilioni, zikiwemo HPLC mbili, GC moja na GC-MS/MS mbili.
Mashine hizo zina uwezo wa kuchakata zaidi ya sampuli 2,000 kwa wiki, huku mashine nyingine nne zenye thamani ya Sh2.1 bilioni zikitarajiwa kufungwa ifikapo Septemba 2026.
TPHPA pia imenunua magari 18, pikipiki 38, drones 21, vishikwambi 41 na portable DNA sequencers 19, pamoja na ndege maalumu ya kunyunyizia viuatilifu aina ya Thrush 510P2+, yenye uwezo wa kubeba hadi lita 1,930 za kiuatilifu.
MAPATO YAONGEZEKA
Katika upande wa mapato, TPHPA ilikuwa na lengo la kukusanya Sh43 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo hadi Mei 2026 ilikuwa imekusanya Sh35.2 bilioni, sawa na asilimia 82 ya makadirio ya mwaka.
Kutokana na makusanyo hayo, Mamlaka iliingiza Sh2.9 bilioni katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Aidha, mapato katika baadhi ya vituo vya mipakani yaliongezeka kutoka Sh14.49 bilioni katika kipindi cha kabla ya maboresho hadi Sh89.18 bilioni katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026.
MWELEKEO 2026/2027
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, TPHPA imeweka mkazo katika kufungua masoko mapya, kulinda masoko yaliyopo, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa mazao (traceability), kufanya Pest Risk Analysis (PRA) na kuongeza idadi ya kampuni zinazokidhi masharti ya masoko ya kimataifa.
Mamlaka pia itaendelea kuimarisha maabara na huduma za afya ya mimea katika Kurasini, Tabora, Njombe na Mtwara, huku ujenzi wa maabara ndogo ukiendelea katika vituo 47 vya mipakani.
Kwa ujumla, TPHPA imesema uwekezaji katika afya ya mimea, teknolojia, udhibiti wa visumbufu na usalama wa viuatilifu unaendelea kuwa msingi wa kuongeza uzalishaji, kupunguza hasara kwa wakulima, kulinda afya ya walaji na kufungua masoko mapya ya kimataifa kwa mazao ya Tanzania.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/3KbTI4X
Tags
News

