Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed akiwa katika banda mojawapo la maonesho ya biashara na uwekezaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga DC yenye kauli mbiu isemayo" Mbinga DC, eneo la fursa, mahali salama pa Kuwekeza. 

Na Regina Ndumbaro, Mbinga-Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia teknolojia za kisasa katika kutangaza bidhaa, kutafuta masoko, kuhifadhi taarifa na kuwasiliana na wateja ili kupanua shughuli zao za biashara.
Wito huo umetolewa wakati wa kufunga Maonesho ya Biashara na Uwekezaji ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga yaliyofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 24 hadi 27, 2026 katika ukumbi wa Mbinga DC Mall, yakibeba kaulimbiu “Mbinga DC, Eneo la Fursa, Mahali Salama pa Kuwekeza.”
Brigedia Jenerali Ahmed amesema biashara haiwezi kutenganishwa na teknolojia, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali kama nyenzo muhimu ya kutangaza bidhaa na huduma zao, kutafuta masoko mapya na kuwasiliana na wateja.
Amesema matumizi ya teknolojia yanaweza kuwawezesha wafanyabiashara kuvuka mipaka ya maeneo wanayofanyia biashara na kuwafikia wateja waliopo katika mikoa mingine ndani ya Tanzania na hata masoko ya kimataifa.
Amesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kuonesha bidhaa, huduma, teknolojia na ubunifu unaopatikana katika maeneo yao, huku akieleza kuwa amepita katika mabanda mbalimbali na kujionea ubunifu, vipaji na utayari wa wafanyabiashara katika kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amepongeza kikundi cha utamaduni kilichotumbuiza kwa kuimba nyimbo zilizoeleza uzuri na fursa zilizopo katika Wilaya ya Mbinga.
Brigedia Jenerali Ahmed amewataka wafanyabiashara kuendelea kuboresha bidhaa na huduma zao kwa kuzingatia ubora, ushindani, ubunifu na ufungashaji, huku wakitumia teknolojia katika kukuza masoko.
Amesema Ruvuma ina fursa katika kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, viwanda vidogo, utalii, madini, huduma za teknolojia na sekta nyingine za uzalishaji, hivyo ni muhimu kutumia teknolojia kuutangaza uwezo huo na kuwafikia walaji na wawekezaji walioko maeneo mbalimbali.
Aidha, amewasihi wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia teknolojia kwa ajili ya kutangaza bidhaa, kutafuta masoko, kuhifadhi taarifa na kuwasiliana na wateja, akisisitiza kuwa mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali ni sehemu muhimu ya kupanua masoko.
Amesema maonesho hayo yameonesha pia uwezo wa vijana na wanawake katika shughuli za biashara na uzalishaji, hivyo taasisi zinazohusika na uwezeshaji wa kiuchumi zinapaswa kuendelea kutoa elimu ya biashara, ujuzi wa ujasiriamali, huduma za kifedha na ushauri ili kuwawezesha kutumia fursa zilizopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura, amesema mwitikio wa maonesho hayo umekuwa mkubwa, huku jumla ya washirika 51 wakishiriki, wakiwemo baadhi ya wawekezaji kutoka Njombe na Moshi.
Amesema maonesho hayo yalilenga kuwapa fursa wafanyabiashara, wajasiriamali, taasisi za Serikali na fedha, vikundi vya kiuchumi na wadau mbalimbali kuonesha bidhaa na huduma zao, kutoa elimu kuhusu biashara na uwekezaji, elimu ya fedha na huduma za kifedha, pamoja na kuwasilisha fursa za biashara na uwekezaji zilizopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kisari Makole, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi na wawekezaji kufanya shughuli zao kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria, taratibu na mipango ya maendeleo.








from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/PLzNGQ4
