PROF. SHEMDOE ASHIRIKI MAFUNZO YA UONGOZI HARVARD KUIMARISHA UWEZO WA UONGOZI, UTEKELEZAJI WA SERA



Na Mwandishi Wetu, Boston - Marekani

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, anashiriki  mafunzo maalum ya uongozi kwa Mawaziri wa Kisekta yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Harvard, jijini Boston, Marekani.

Mafunzo hayo ya siku nne yameanza Septemba 26, 2026 na yanatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2026, yakilenga kuwawezesha Mawaziri wa Kisekta kutoka nchi mbalimbali za Afrika na maeneo mengine kubadilishana uzoefu na maarifa katika uongozi, usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya wizara za kisekta.

Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Mawaziri wa Kisekta kutoka Tanzania, Kenya, Nigeria, Namibia, Chile, Dominican Republic, Malawi, Benin, Côte d’Ivoire, Gabon, Ghana, Guinea, Mauritius, Mauritania, Msumbiji, Sierra Leone na Togo.

Kupitia mafunzo hayo, Mawaziri hao wanapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu mbalimbali za uongozi wa kisekta, usimamizi wa taasisi za umma, ufanyaji wa maamuzi na namna ya kuimarisha utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, mafunzo hayo yanawapa washiriki fursa ya kujifunza kutoka kwa viongozi wenye uzoefu mkubwa, wakiwemo Mawaziri wa zamani na Marais wastaafu, pamoja na kushirikishana uzoefu kuhusu changamoto na fursa zinazojitokeza katika uongozi wa sekta za umma.

Miongoni mwa wakufunzi katika mafunzo hayo ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na Rais wa Tano wa Botswana, Mhe. Mokgweetsi Masisi.

Ushiriki wa Prof. Shemdoe katika mafunzo hayo unatoa fursa ya Tanzania kushiriki katika jukwaa la kimataifa la kubadilishana uzoefu wa uongozi na usimamizi wa sekta za umma, hususan katika maeneo yanayohusu Serikali za Mitaa na utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa wananchi.

Maarifa na uzoefu unaopatikana kupitia mafunzo ni nyenzo muhimu katika kuendelea kuimarisha uongozi, usimamizi na utoaji wa huduma za Serikali kwa ufanisi, pamoja na kuongeza ujuzi wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya kisekta pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kozi hiyo  imeandaliwa na T.H. Chan School of Public Health, Harvard Graduate School of Education na Harvard Kennedy School, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha viongozi wa kisekta kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu katika uongozi wa umma.









from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/LDHogqh

Post a Comment

Previous Post Next Post