Mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba na awali katika shule ya Ajofu na Brilliant iliyopo Kata ya Subira Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma James Mgongolwa Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma
Wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Ajofu na Brilliant iliyopo Kata ya Subira, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameipongeza shule hiyo kwa mchango wake katika kuwajenga wanafunzi kitaaluma na kimaadili, wakieleza kuwa ufaulu mzuri wa wanafunzi hao ni matokeo ya juhudi za walimu pamoja na ushirikiano wa wazazi.
Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2016 ikiwa na wanafunzi wanane na walimu watatu, imeendelea kukua na katika mahafali hayo imehitimisha wanafunzi 42, wakiwemo 33 wa darasa la awali na tisa wa darasa la saba.
Katika risala yao iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi wa mahafali hayo, James Mgongolwa kwa niaba ya Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Songea, wanafunzi wamewaomba wazazi na walezi kuongeza ufuatiliaji wa maendeleo na mienendo ya watoto wao shuleni, pamoja na kushirikiana kwa karibu na walimu.
Wamesema wazazi wanapaswa kupunguza muda mwingi wanaoutumia kwenye simu na kuzingatia ukuaji, malezi na maendeleo ya watoto wao, huku wakisisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja kati ya wazazi na walimu ni muhimu katika kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo.
Aidha, wanafunzi hao wamemuomba mgeni rasmi na viongozi husika kusaidia kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara inayounganisha shule hiyo na mjini, wakieleza kuwa barabara hiyo huwa mbovu na haipitiki vizuri wakati wa msimu wa masika.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mgongolwa amesema amesikia kilio hicho na amekipokea, hivyo atakifikisha katika sehemu husika kwa hatua zaidi.
Pia amewataka wazazi kuwa karibu na watoto wao na kufuatilia kila hatua ya ukuaji na maendeleo yao, akisema bila ufuatiliaji wa karibu watoto wanaweza kushindwa kutimiza wajibu wao, huku akiwakumbusha wahitimu kuwa elimu yao ndiyo kwanza inaanza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Ajofu na Brilliant, Mwalimu Hekima, amewataka wahitimu kwenda kuwakilisha vyema shule yao katika hatua nyingine za elimu, akisema walimu wametumia muda mwingi kuwalea na kuwajenga kitaaluma na kimaadili.
Amewasisitiza kumtanguliza Mungu katika kila jambo watakalolifanya ili waweze kufanikiwa.
Wazazi waliohudhuria mahafali hayo wameendelea kupongeza walimu kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuwafundisha watoto wao, hususan katika taaluma na maadili, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na shule katika malezi na maendeleo ya wanafunzi.







from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/PoCxeNJ

