Atlas Schools Marathon 2026 kumuenzi Mwl.Nyerere kwa kuhamasisha Jamii Kutunza Mazingira


Na Mwandishi Wetu

ATLAS Schools inatarajia kushirikisha zaidi ya wakimbiaji 3,000 katika mbio za Atlas Schools Half Marathon, msimu wa nane, zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 14, mwaka huu, katika viwanja vya shule hiyo, Madale, Dar es Salaam, kwa lengo la kuhamasisha afya bora, michezo na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mbio hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Atlas Day, Wakili Didas Kanyambo, amesema tukio hilo linatarajiwa kuvutia zaidi ya watu 10,000 watakaoshiriki kwa namna mbalimbali, likiwa na kaulimbiu isemayo “Run for Nature, Run for Kids” inayosisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa manufaa ya watoto na vizazi vijavyo.

Amesema mbio hizo zitakuwa na makundi matatu, yakiwamo kilomita 21 kwa wanariadha wa mbio ndefu, kilomita 10 kwa kampuni na taasisi, pamoja na kilomita tano kwa washiriki wanaotaka kushiriki kwa burudani na kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi. Ameeleza kuwa njia za mbio zimeandaliwa kwa kuzingatia umbali na usalama wa washiriki.

Kanyambo amesema kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha jamii kutambua kuwa afya na maendeleo ya watoto yanategemea pia mazingira wanamoishi, yakiwamo upatikanaji wa hewa safi, maji salama, miti na maeneo safi. Ameongeza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja, kuanzia familia, shule na taasisi hadi Serikali na sekta binafsi.



Amesema Oktoba 14 pia itakuwa siku ya mahafali ya 20 ya Atlas Schools, yatakayowakutanisha wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la saba na kidato cha nne. Amesema kuunganisha mbio hizo na mahafali ni sehemu ya utamaduni wa shule hiyo wa kuenzi Siku ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kuhimiza elimu, nidhamu, uzalendo na malezi bora kwa watoto.

Kwa mujibu wa Kanyambo, Atlas Schools inaamini kuwa elimu bora haipaswi kuishia katika ufaulu wa mitihani pekee, bali inapaswa kumjenga mwanafunzi katika nyanja mbalimbali, zikiwamo michezo, afya, uongozi na utunzaji wa mazingira. Amesema shule hiyo inasisitiza ufaulu wa kiwango cha Single Digit huku ikiweka mazingira yanayowezesha wanafunzi kukuza vipaji na kujiandaa kwa maisha ya baadaye.

Katika mbio hizo, washindi watano wa kwanza katika kila kundi watapata zawadi za fedha kwa wanaume na wanawake. Mshindi wa kwanza wa kilomita 21 atazawadiwa Shilingi 300,000, kilomita 10 Shilingi 200,000 na kilomita tano Shilingi 150,000, huku zawadi nyingine zikitolewa kulingana na nafasi za washindi. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa zawadi ni Shilingi 3,010,000.

Amesema ada ya ushiriki ni Shilingi 40,000, ambapo kila mshiriki atapata vifaa rasmi vya kukimbilia (Official Running Kit) pamoja na medali baada ya kumaliza mbio. Usajili na malipo yatafanyika kupitia MIXX by YAS Paybill namba 5927380, kwa jina la Atlas Schools, huku washiriki wenye changamoto wakitakiwa kuwasiliana na uongozi kupitia namba 0787 651 656 au 0715 651 656.

Aidha, amewashukuru wadhamini na washirika wa mbio hizo, wakiwamo Kilimanjaro Natural Mineral Water, SGA Security, ASAS Maziwa, Kuambiana Investment, 4JS Fitness Centre, CRDB Bank na Riadha Taifa, kwa kuunga mkono maandalizi. Amewahimiza wananchi, kampuni, taasisi, wazazi na vijana kujisajili mapema na kushiriki katika mbio hizo, akisisitiza kuwa ujumbe mkuu ni kulinda mazingira leo ili watoto warithi Tanzania safi na salama kesho.

Post a Comment

Previous Post Next Post