
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi amesema kukamilika kwa mradi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Malangali, mkoani Rukwa, kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi kwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuvutia wawekezaji na kuwezesha Tanzania kuuza umeme Mataifa Jirani.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, Makamu wa Rais amesema Mkoa wa Rukwa wenye mahitaji ya takribani megawati 30, kwa sasa unapokea megawati 16 pekee, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za uzalishaji, hususan uchakataji wa mazao ya kilimo na madini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika mradi huo ili kuhakikisha Rukwa inaunganishwa na Gridi ya Taifa na kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Leo hii TANESCO inanunua umeme Zambia, lakini kwa laini hii sisi tutaanza kuiuzia Zambia umeme mkubwa na wa uhakika,” amesema Makamu wa Rais, huku akiwataka wa wawekezaji kuchangamkia fursa za kiuchumi mkoani Rukwa na wananchi kulinda miundombinu hiyo.


