RAIS SAMIA ATOA SHILINGI BILIONI 31.4 KUKARABATI BARABARA YA GEHANDU – BABATI



Na Mwandishi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa Shilingi bilioni 31.41 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa matengenezo ya kilomita 66.5 za Barabara Kuu ya Gehandu–Babati, yenye urefu wa jumla wa kilomita 105.5. Barabara hiyo ni kiungo muhimu cha usafiri kati ya Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Singida.

Fedha hizo zinatumika katika matengenezo yanayotekelezwa kwa awamu, yakiwemo kuziba mashimo, kurekebisha maeneo korofi yenye uharibifu na kuweka tabaka jipya la lami (resealing), pamoja na ukarabati wa sehemu zilizoathirika (partial rehabilitation), kulingana na kiwango cha uharibifu.

Akizungumza leo, Oktoba 25, 2026, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya kazi za ukarabati wa barabara hiyo.

Amesema barabara hiyo hutumiwa na idadi kubwa ya magari, hususani magari makubwa ya mizigo yanayosafirisha mazao ya kilimo, madini na bidhaa nyingine kutoka Bandari za Tanga na Mombasa kwenda maeneo mbalimbali nchini na katika nchi jirani, zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Aidha, Mhandisi Besta ameeleza kuwa Serikali, kupitia Kitengo cha Tafiti na Maendeleo (RDU), imekamilisha utafiti na kushauri kuwa barabara hiyo inahitaji kujengwa upya kwa kuwa imefikia mwisho wa muda wake wa usanifu (End of Design Life).

Kuhusu maendeleo ya utekelezaji, amesema mpango wa matengenezo unahusisha kilomita 66.5, zilizogawanywa katika sehemu nne. Sehemu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 15 imekamilika kwa asilimia 100, huku sehemu ya pili yenye urefu wa kilomita 20 ikiwa imefikia asilimia 17 ya utekelezaji.

Ameongeza kuwa sehemu zilizobaki zinaendelea kuandaliwa kwa ajili ya utekelezaji, ambapo makandarasi wamepatikana na wanaendelea na maandalizi ya kupeleka mitambo na vifaa vya ujenzi maeneo ya kazi.

Kwa mujibu wa mpango huo, sehemu ya kwanza na ya pili zenye jumla ya kilomita 35 zinatekelezwa na Mkandarasi M/s Saimoo Co. Ltd. Sehemu ya tatu, yenye urefu wa kilomita 15, ipo kati ya Dareda na Masqaroda na inatekelezwa na Mkandarasi M/s Rocktronic Ltd. Sehemu ya nne, yenye urefu wa kilomita 16.5, ipo kati ya Katesh Mjini na Masqaroda na inatekelezwa na Mkandarasi M/s Saimoo Co. Ltd.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Hanang, Mhe. Asia Halamga, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo hususani maeneo korofi.

Mbunge Halamga amesema kuwa kukamilika kwa sehemu ya kwanza na kuendelea kwa kazi katika sehemu ya pili ni hatua muhimu katika kuboresha hali ya barabara hiyo.

Kwa kauli moja, wananchi wa Wilaya ya Hanang wamemshukuru Rais kwa kuwezesha ukarabati huo, wakieleza kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa Watanzania kwa ujumla na kwa wakazi wa Hanang hususani, kutokana na mchango wake katika usafirishaji wa mazao ya kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi.

Utekelezaji wa matengenezo hayo unalenga kuboresha hali ya barabara, kuongeza usalama wa watumiaji, kupunguza gharama za uendeshaji wa magari na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika ukanda huo muhimu wa kiuchumi.









from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/nhZFV87

Post a Comment

Previous Post Next Post