
Na: OWM–TAMISEMI, Makambako
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali itapeleka shilingi milioni 600 katika Halmashauri ya Mji wa Makambako kabla ya Desemba 2026 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kitandililo, hatua itakayosaidia kusogeza huduma bora za matibabu karibu na wananchi.
Prof. Shemdoe ameyasema hayo Oktoba 17, 2026, akiwa Makambako, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, kueleza hatua zinazochukuliwa na OWM-TAMISEMI kuboresha huduma za afya ya msingi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika wakati wa ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Njombe.
“Mhe. Makamu wa Rais, tumeshapata shilingi milioni 600 ambazo tutazileta hapa Makambako kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kitandililo kabla ya Desemba, ili wananchi wapate huduma bora za matibabu kwa wakati,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Kuhusu ombi la Mbunge wa Makambako ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, la kujenga zahanati mbili, Prof. Shemdoe amesema ofisi yake inaendelea kulifanyia kazi kwa kutafuta fedha ili zitakapopatikana zitumike kujenga zahanati hizo na kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema anatambua jitihada zilizofanywa na Naibu Waziri wa OWM-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Mhe. Dkt. Festo Dugange, pamoja na Waziri wa Nchi, OWM-TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, wakati akiwa Katibu Mkuu, katika kusimamia ujenzi wa Shule ya Mkoa ya Wasichana ya Sayansi ya Vipaji Maalumu iliyojengwa Wanging’ombe.
Ujenzi wa Kituo cha Afya Kitandililo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa kupunguza vifo vya mama na mtoto, gharama za matibabu na usafiri, huku ukiimarisha afya ya jamii, kuongeza tija na uzalishaji, na kujenga rasilimali watu yenye afya kwa maendeleo endelevu ya taifa.






from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/T7X8hat
Tags
News
