Jumamosi, Novemba 21, 2026,
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewataarifu wateja wake katika Mikoa ya Mbeya na Songwe kuwa kumetokea ajali ya kuanguka kwa nguzo kubwa ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 inayohusiana na Mradi wa TAZA, ambayo imeangukia miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 220 inayosafirisha umeme kutoka Iringa kwenda Mbeya, katika eneo la Inyala mkoani Mbeya.
Kutokana na ajali hiyo, huduma ya umeme imekatika katika Mikoa ya Mbeya na Songwe. TANESCO imeeleza kuwa wataalamu wa shirika hilo tayari wamefika katika eneo la tukio na wanaendelea na jitihada za kurekebisha miundombinu iliyoathirika ili kuhakikisha huduma ya umeme inarejea katika hali ya kawaida.Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa uharibifu uliotokea, kuna uwezekano wa kuchelewa kwa kurejea kwa huduma ya umeme. Shirika limeahidi kuendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya kazi za ukarabati na hatua zinazochukuliwa kurejesha huduma hiyo.
Aidha, TANESCO imeomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza na kuwaomba wateja wote katika Mikoa ya Mbeya na Songwe kuwa na uvumilivu wakati wataalamu wake wakiendelea kushughulikia changamoto hiyo.
Taarifa hii imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Huduma kwa Wateja ya TANESCO, Makao Makuu, Dodoma.


