Mkurugenzi
wa shirika la ujasusi la Marekani Bi Gina Haspel atafanya mahojiano na
wajumbe wa bunge la Congress juu ya mauaji ya mwanahabari Jamal
Khashoggi.
Vyombo vya habari nchini Marekani vinaripoti kuwa bi Haspel atakutana na viongozi wa bunge la Seneti baadae leo Jumanne.
Mkurugenzi huyo hakuwepo wiki iliyopita wakati mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi walipofanya mazungumzo na viongozi wa Seneti, kitendo ambacho kiliwakasirisha baadhi ya wajumbe wa bunge hilo.
Khashoggi
aliuawa ndani ya ofisi za ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini
Istanbul, Uturuki Oktoba 2. Mwanahabari huyo alikuwa ni mkosoaji mkubwa
wa sera za Saudia hususani mwanamfalme Mohammed bin Salman.
Vyombo
vya habari vya Marekani pia vimeripoti kuwa ripoti ya CIA juu ya mkasa
huo inaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa bin Salman aliamuru mauaji
hayo.
Tayari Saudia imewashitaki watu 11 juu ya mauaji hayo, lakini wanakanusha vikali juu ya uhusika wa bin Salman.
Tags
matukio

