Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amewahakikishia wananchi wa
baadhi ya vijiji ambavyo havina mawasiliano mkoani Lindi na Pwani kuwa Serikali
ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. John
Pombe Magufuli inahakikisha kuwa wananchi waishio kwenye vijiji hivyo wanapata
huduma za mawasiliano ya uhakika
Nditiye ameyasema hayo
akiwa kwenye ziara yake ya kukagua changamoto za hali ya upatikanaji wa huduma
za mawasiliano kwa wananchi waishio maeneo ya Liwale, Lindi Vijijini, Mtama,
Kibiti na Rufiji kwenye mkoa wa Lindi na Pwani baada ya kupata kilio kutoka kwa
wabunge wanaowakilisha wanananchi wa maeneo hayo wakati wa kikao cha Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania cha mwezi Novemba mwaka huu
Amesema kuwa Sekta ya
Mawasiliano ni sekta inayoshika nafasi ya pili kwa kuchangia pato la taifa
katika kipindi cha mwaka 2016/2107 kwa kiwango cha asilimia 13.1 ambapo
mawasiliano yana changui kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa letu na
mawasiliano ndiyo kila kitu. “Wananchi mkiwasiliana kwa kununua vocha, kupiga
simu na kutumia intaneti, Serikali inatoza kodi kidogo, ambayo wala haiumizi na
wala mwananchi hausikii, lakini Serikali inapata mapato yake,” amesema Nditiye.
Amefafanua kuwa ni
muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma za
mawasiliano ambapo hadi sasa asilimia 94
ya wananchi wote wanawasiliana kwa kuwa Serikali imeanzisha Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao unatoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi
ili ziweze kupeleka huduma za mawasiliano kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa
kibiashara
Mkuu wa Wilaya ya
Liwale Sara Chiwamba amemshukuru Nditiye kwa ziara yake Liwale na kufika Mirui
kuzungumza na wananchi ambao wana kiu ya kupata mawasiliano. “Tuna imani
mawasiliano yatapatikana kwa kuwa mawasiliano yanasaidia ulinzi na usalama na
Wilaya yetu itaenda kufunguka,” amesema Chiwamba.
Naye Mbunge wa Liwale
Zuberi Kuchauka amemweleza Nditiye kuwa mradi huu wa mawasiliano kwenye kata ya
Mirui ni miongoni mwa miradi sita inayotekelezwa na UCSAF na ni matumaini kuwa
hadi Januari 2019, Mirui watakuwa wameunganishwa na dunia kupitia mawasiliano.
Pia ameongeza kuwa anamshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kujipambanua
kuwa ni Rais wa Serikali ya wanyonge, “kweli tunaona anawatetea wanyonge na
anatembea kwenye kauli yake, tunashukuru amewakomboa wakulima wa korosho,”
amesisitiza Kuchauka
Vile vile, Mkuu wa
Wilaya la Lindi Shaibu Ndemanga amemshukuru Nditiye kwa kufika na kufanya
mkutano na wananchi wa kijiji cha Chihuta kilichopo Mtama, Lindi kwa kuwa
wamekosa mawasiliano kwa muda mrefu angali wana uchumi mzuri wa korosho.
Nditiye amesema kuwa, “nitafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa
wananchi wa Chihuta mnapata mawasiliano kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni
maendeleo,”. Nditiye ameilekeza UCSAF
ifike Chihuta ndani ya mwezi mmoja ifanye utafiti na kujenga mnara wa
mawasiliano. Pia ameongeza kuwa kwenye jimbo la Mtama ipo miradi nane ya
mawasiliano na miradi mingine sita inaongezwa na mwezi Machi mwakani na zabuni
nyingine itatangazwa na UCSAF ili kampuni za simu ziweze kuomba kwa lengo la
kujenga minara ya kufikisha huduma za mawasiliano ili wananchi wawasiliane
Pia ametembelea na
kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na changamoto zilizopo kwa
wananchi katika maeneo ya Mbuchi na
Mchukwi Wilayani Kibiti ambapo amebaini uwepo wa ukosefu wa mawasiliano ya
uhakika kwa wananchi waishio maeneo hayo na wanaofika kupata huduma kwenye
hospitali ya Mchukwi ambapo amebaini kuwa Kampuni ya Halotel ilifika na kufanya
tathmini ya kujenga minara kwenye baadhi ya maeneo hayo ambapo imechukua muda
bila kurejea na kukamilisha kazi hiyo.
Nditiye ameielekeza
UCSAF iwasilishe ofisini kwake ndani ya wiki moja orodha ya minara inayoendelea
kujengwa, ambayo imesimama kujengwa kwa kipindi cha miezi sita hadi sasa na
ambayo haijaanza kujengwa. Pia, UCSAF ihakikishe kampuni za simu zinaongeza
nguvu ya mawasiliano kwenye minara ya maeneo ya Mchukwi ili wananchi waweze kupata
mawasiliano ya uhakika nyakati zote
Naye Mbunge wa Kibiti
Ali Seif Ngando amemhakikishia Nditiye kuwa mnara ukikamilika watautunza kwa
kuwa utawasaidia wananchi kupata masoko ya bidhaa na fursa mbali mbali. Pia,
Mkuu wa Wilaya hiyo Gullam-Hussein Shaban Kifu amemuomba Nditiye awasaidie ili
kampuni ya Vodacom iweze kufika kwenye Hospitali ya Mchukwi ili waongeze nguvu
ya mawasiliano ya mnara wao ili wananchi, wagonjwa na wataalam wa tiba
wanaotoka nje ya nchi kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwenye hospitali hiyo
waweze kupata mawasiliano na huduma za intaneti
Naye mwakilishi wa
Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF Mhandisi John Mukondya amekiri uwepo wa ukosefu na
changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye maeneo hayo na
amepokea maelekezo ya Nditiye ili kuhakikisha kuwa wanafika maeneo hayo kwa
kushirikiana na kampuni za simu kufanya utafiti ili kujenga minara ya
kuwawezesha wananchi kuwasiliana
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
