Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constanine
Kanyasu ametoa wito kwa wafanyabiashara
za utalii nchini kuwekeza katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini ambayo ina vivutio vingi vya utalii.
Pia, Amesema kuwa wizara yake itaendelea kuweka mazingira
rafiki kwa wafanyabiashara hao kwa
kupunguza masharti kwa kampuni binafsi za utalii hasa za wazawa ili kuongeza
tija katika biashara ya utalii nchini.
Amebainishwa hayo wakati Naibu Waziri huyo akifungua Maonesho ya tatu ya Utalii ya Karibu Kusini yanayofanyika katika
viwanja vya Kichangani mkoani Iringa yenye kauli mbiu isemayo’’ Karibu Kusini
Ufurahie Utalii Wetu’’
Akitaja mikoa hiyo ya Nyanda ya juu kusini kuwa ni Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Ruvuma, Rukwa
na Katavi, Mhe. Kanyasu amesema kuwa mikoa hiyo imejaliwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya
kihistoria, kiutamaduni na kiikolojia vinavyofanya upekee wa mikoa hiyo katika sekta ya utalii hapa nchini na
ulimwenguni.
Sambamba na hilo, Mhe. Kanyasu amewataka wafanyabishara
hao waanze kuwekeza miundombinu ya
utalii kama vile kujenga hoteli pamoja
na kufungua kampuni za utalii katika ukanda huo badala ya kuendelea kuwekeza zaidi
katika mikoa ya Kaskazini.
Katika hatua nyingine,Mhe,Kanyasu ameiagiza Mikoa yote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza vivutio vya utalii
ikiwa pamoja na kuvitunza kuvitangaza
vivutio hivyo.
Aidha, Mhe, Kanyasu
amewasihi Wakuu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo kwa pamoja na kuwa na vikao vya mara kwa mara na
wadau wa utalii katika Mikoa hiyo ili kuimarisha
maendeleo ya sekta ya utalii katika mikoa hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bw. Richard Kasesela
amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) imeitenga mikoa
hiyo kwa vile katika maonesho ya Utalii ya Nje za nchi, TTB imekuwa
haivitangazi vivutio vilivyoko Nyanda za Juu Kusini.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa huyo amemuomba Naibu Waziri
Mhe. Kanyasu aiagize TTB itoe kipaumbele kwa kutangaza vivutio vya mikoa hiyo
katika maonesho ya ndani na nje ya nchi
ili vivutio wa mikoa hiyo viweze kujulikana
kama vivutio vya mikoa ya
kaskazini.
Maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini yalizinduliwa mwaka 2016 yakiwa yamelenga kuchochea
maendeleo ya utalii kwa Mikoa ya Kusini kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo
katika mikoa hiyo.
