Serikali imezitaka taasisi zote ambazo bado
hazijajiunga na Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
(GePG) kuhakikisha wamejiunga na mfumo huo kabla ya Juni 30, 2019.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo Bw. Doto James, wakati wa Mkutano wa mwaka wa wadau wa utumiaji wa mfumo wa GePG Jijini
Dodoma.
Dkt. Kazungu, alisema kuwa hakutokuwa na fedha yoyote ya umma
itakayokusanywa nje ya Mfumo wa GePG, hivyo wakati mwafaka wa kujiunga na
kuunganishwa na mfumo huo ni sasa.
“Napenda kusisitiza kuwa, ni lazima kutumia mfumo
huu kwa kuwa unaongeza ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa Fedha za Umma na
pia utaratibu wa matumizi ya GePG unatoa
fursa ya kuwa na njia nyingi za kulipia na kuwapa walipaji wa huduma za Serikali
utaratibu rafiki wa kufanya malipo”, alieleza Dkt. Kazungu.
Utaratibu wa makusanyo kabla ya mfumo wa GePG haukua rafiki kwa kuwa ilikuwa ni vigumu kuthibitisha
malipo na pia kuwa na foleni ndefu
kwenye Ofisi za Serikali zilizosababishwa na zoezi la kufanyiwa tathmini ya
malipo ya huduma na kuthibitisha malipo.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo katika
ukusanyaji wa Fedha za Umma, Juni 2017, Serikali iliifanyia marekebisho Sheria
ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka 2001 na kuongeza kipengele kinachotaka Fedha
zote za umma zikusanywe kupitia Mfumo wa Government e-Payment Gateway (GePG).
Lengo la kuanzishwa kwa GePG ni kutatua changamoto
zilizopo kwenye Mfumo uliokuwepo wa ukusanyanji wa fedha za umma ili kuongeza uwazi
na udhibiti wa fedha za umma, kuboresha na kurahisisha namna ya kulipia huduma
za umma na pia kupunguza gharama zinazoambatana na ukusanyaji wa fedha hizo
ambapo mfumo huo ulianza kutumiwa rasmi na taasisi za umma mwezi Julai 2017 baada
ya majaribio yake kukamilika.
Alisema kuwa utaratibu GePG unaenda sambamba na
utekelezaji wa maelekezo mengine ya Serikali yanayohusu makusanyo ikiwemo yale
yanayotaka akaunti kuu za makusanyo za taasisi za umma kuwepo Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), hivyo ni lazima kuhakikisha akaunti za Taasisi za ummaa za
makusanyo zilizoko Benki Kuu zimewasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha
na mipango ili ziunganishwe na GePG.
Mpaka sasa takribani Benki kumi na moja (11) na mitandao sita(6)
ya malipo kwa njia ya simu za kiganjani zimeshaunganishwa na mfumo huo.
Dkt. Kazungu alisema kuwa ni vyema taasisi za
Serikali kuwa na akaunti za makusanyo kwenye benki zaidi ya moja kati ya benki
zilizoungwa na GePG ili kuwarahisishia walipaji wa huduma za serikali kwa kuwa malipo
yote yanayopitia GePG hayatozwi ada za miamala na benki hizo, hivyo kuongeza
akaunti za makusanyo hakutoongeza gharama za miamala kwa taasisi za umma.
Alibainisha kuwa kutekelezwa kwa rai hiyo kutaondoa
hatari ya taasisi ya umma kukosa huduma ya malipo endapo benki inayotumiwa
itashindwa kutoa huduma kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuvunja makubaliano ya namna
ya kuzihudumia akaunti zilizounganishwa kwenye mfumo wa
Naibu Katibu Mkuu Kazungu amewataka wajumbe wa mkutano huo kuwa chachu katika kuboresha utendaji kwa vitendo kwa kutoa huduma
nzuri kwa wananchi zinazohusisha ukusanyaji wa Fedha za Umma katika maeneo yao
ya kazi baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Kwa upande wake Mkurungezi wa Mifumo ya Fedha wa
Wizara ya Fedha na Mipango Bw. John Sausi, alisema kuwa mfumo huo umekuwa na
tija tangu ulipoanzishwa kwa kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha inaweza
kuona makusanyo yote yanayoingia hivyo kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa
mapato, uwajibikaji na uwazi.
Alisema kuwa, jumla ya Taasisi 326 zimeunganishwa na
Mfumo wa GePG na miongoni mwa Taasisi
hizo ni Wakala wa Misitu, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO)
Amezitaja changamoto za Mfumo huo kuwa ni pamoja na
Benki 11 tu ndizo zinazotumia mfumo huo kati ya Benki zaidi ya 50, hivyo kuleta
mkanganyiko kwa wadau wanaotumia mfumo huo.
Mkutano wa wadau wote wanaotumia Mfumo wa GePG ni wa
kwanza kufanyika nchini ukiwa na lengo la kubaini na kutatua changamoto za
mfumo huo tangu ulipoanzishwa.
