Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amezitaka Benki nchini kushusha viwango vya
riba za mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika
na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya
kujiletea maendeleo yao.
Dkt. Kijaji ameyasema
hayo Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Tawi la Benki Azania, Sokoine, na
kusisitiza kuwa Benki zina nafasi kubwa wa kuisaidia nchi kufikia azma yake ya
kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kukuza mitaji na biashara za wananchi.
Alisema kuwa hivi karibuni
Serikali imechukua hatua madhubuti za kiutawala na kisera ili kuhakikisha kuwa
riba za mikopo katika soko zinapungua, ikiwemo Benki Kuu kutoa mikopo ya muda mfupi kwa
benki za biashara, kushusha
riba kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0.
"Tumepunguza
kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za
biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0, hatua ambazo zimesaidia kupunguza
riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia 17"
aliongeza Dkt. Kijaji
"kama haya yote
yamefanyika, iweje benki ziendelee kutoza riba ya asilimia 17 kwa kisingizio
cha kuogopa mikopo chechefu wakati Serikali kupitia Benki Kuu, imeanzisha kanzi
data ya kuhifadhi na kutoa taarifa ya wakopaji (Credit Reference Bureau
System)" alihoji Dkt. Kijaji
Aidha, Dkt. Kijaji ameelezea kusikitishwa
kwake na hatua ya benki hiyo kuwa miongoni mwa benki 5 zilizofungiwa kwa
kipindi maalum kushiriki katika kuuza na kununua fedha za kigeni baada ya
kukiuka taratibu za biashara hiyo.
" Kisheria,
benki zote za biashara zinatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu kuhusu miamala ya
Soko la Fedha za Kigeni kati ya Mabenki waliyofanya kwa siku lakini Benki yako
ni miongoni mwa benki zilizovunja utaratibu huu, hii niaibu!" alisisitiza
Dkt. Kijaji "
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania Bw.
Charles Itembe, amesema Benki yake imeendelea kufanya vizuri katika soko kwa
kupata faida na kwamba imejipanga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa
wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.
"Benki yetu, mwaka 2017, imetengeneza faida
ya shilingi bilioni 1.81 ikilinganishwa na hasara ya Shilingi bilioni 6
iliyoripotiwa Desemba 2016, na imeongeza rasilimali zake kutoka sh. bilioni 338
hadi bilioni 390" alisema Bw. Charles Itembe.
Alisema
kuwa Benki yake imeongeza kiasi cha mikopo iliyotoa kutoka sh. bilioni 129
mwaka 2016 hadi sh. bilioni 187.7 mwaka
2017, sawa na ongezeko la asilimia 10.23 huku akiba za wateja zikiongezeka
kutoka shilingi bilioni 236 mwaka 2016 hadi sh. bilioni 271 mwaka jana.
