Babati yajipanga kuongeza vyanzo vya mapato kuimarisha uchumi




Na John Walter-Babati

Ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara upo katika hali mbaya kutokana na kushindwa kukusanya mapato yake katika eneo la stendi ambalo ndio tegemezi kwa kipindi cha miezi sita.

Hayo yamebainika katika kikao cha wadau wa maendeleo wa mji wa Babati kilichoketi leo jumanne Januari 8.2019 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo ambapo Makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mfuko wa Halmashauri mwaka 2018-2019   ni shilingi 1,811,327,616  lakini katika kipindi cha nusu mwaka kuanzia July hadi Disemba imekusanya shilingi 687,359,057 sawa na asilimia 38.

“Tumeshuka katika ukusanyaji wa mapato kutokana na kunyang’anywa stendi ya mabasi ambayo ndio ilikuwa chanzo kikubwa cha makisio katika bajeti yetu ya mwaka 2018-2019”.

Akisoma taarifa ya mpango wa bajeti wa mwaka 2019 -2020, mchumi wa mji wa Babati Hamisi Katambi amevitaja vyanzo vilivyoongeza makusanyo ni leseni za biashara kwa asilimia 74,mnada shilingi 15,278,400 asilimia 77,ushuru wa huduma shilingi 70,987,165 asilimia 71 huku vyanzo vilivyokusanywa kwa kiwango cha chini  ni ushuru wa wa stendi kwa asilimia 0,vyoo vya umma 0% na maji taka 0%.

Mchumi huyo  amesema  katika mpango na bajeti ya mwaka 2019/2020 Halmashauri imepanga kufanya mabadilko makubwa kwa kuwekeza kwenye Miradi itakayoongeza mapato kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii.

Mfanyabiashara wa kampuni ya Ango  East Afrika Anna Uffoo amesema ni muda mrefu wanakaa vikao vya kushauriana mara kwa mara lakini hakuna mabadiliko yanayofanywa na Halmashauri.

“Katika kikao kilichopita tulizungumza kuhusu ujenzi wa vibanda katika kituo kipya cha mabasi, tulikubaliana kujenga vibanda vya kudumu na sio vya mabati lakini makubaliano hayo hayajatekelezwa na hatujui ni kwanini na nani anatukwamisha”alisema Ufoo

Aidha katibu wa Chama cha wafanyabiashara,wakulima na wenye viwanda mkoa wa Manyara [TCCIA] Mwanahamisi Hussein wa [TCCIA] mkoa wa Manyara Bi Mwanahamisi ameshauri ugawaji wa vibanda katika stendi mpya uzingatie wafanyabiashara waliokuwepo katika stendi ya zamani na sio kufanya kama mchezo wa kamari kwani itapelekea wengi kuacha biashara na kuisababishia halmashauri na serikali hasara katika kukusanya kodi.

Naye mkurugenzi wa asasi binafsi inayoshugulika na uhifadhi wa Wanyama na Mazingira ya Rafiki Wild Life Foundation Mchungaji Clement Matwiga ameishauri Halmashauri iangalie namna ya kulitumia ziwa Babati katika kuongeza mapato ya mji kwa kudhibiti uvuaji wa samaki kiholela na kutoa elimu kwa wavuvi ili waweze kulipa ushuru pamoja na  kutengeneza mazingira yatakayokuwa yakitembelewa na watu mbali mbali kupiga picha za kumbukumbu.

from MUUNGWANA BLOG http://bit.ly/2C5djbw

Post a Comment

Previous Post Next Post