Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkao wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuanzia Februari Mwaka huu Dar es Salaam litakuwa jiji la biashara rasmi kwa kuruhusu kufanyika shughuli usiku na mchana bila kulala.
Alisema hayo ofisini kwake jana, wakati akitoa tahmini ya mipango yake kuhusu wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi na kufaulu, ambapo ameahidi wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari za serikali watapata nafasi.
Aidha, kuhusu kufanya shughuli za biashara saa 24 Makonda alisema kwa kuwa Rais Dk. John Magufuli alishazungumza anataka kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji la biashara hivyo hakuna budi biashara zifunguliwe muda wote ikiwemo Bar.
“Februari mwaka huu tutaruhusu wafanyabiashara kufanya kazi saa 24 ikiwemo wamiliki wa Bar. Si kwa ajili ya Bar tu tuna mpango wa kuhakikisha Dar es Salaam inafanya kazi saa 24, Rais ameshatangaza Dar es Salaam itakua jiji la biashara, hatuwezi kuwa jiji la biashara ikiwa watu wanenda kulala,” alisema Makonda.
Alibainisha kuwa, “Nitahakikisha Dar es Salaam linakua jiji la usiku na chana. Si muda mrefu tutakutana na wafanyabiashara wote, wenye maduka wenye shopping Mall na wenye Bar, nina uhakika haitafika mwezi wa pili nitahakiksha Dar itakua jiji la biashara. Nenda zako Kariakoo saa nne hadi saa saba usiku, fanya manunuzi yako kisha safari. Tumeongea ongea sana lakini sasa ni wakati wa utekelezaji.”
Katika hatua nyingine Makonda alisema, anahakikisha ujenzi na ukarabati wa madarasa 622 unakamilika kwa wakati, lengo la kufanikisha wanafunzi 31,092 ambao ni sawa na asilimia 47 ya watoto 64,861 waliofaulu katika mkoa huo wanaendelea na masomo yao ya kidato cha kwanza.
Alisisitiza, lengo kuu ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi yoyote ambaye ataachwa kwa sababu ya kigezo cha uhaba wa madarasa, kwa sababu mkoa wake una rasilimali zote za kuwafanya wanafunzi wasome kwa amani na utulivu.
Alidai, wanafunzi wote waliofaulu katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana watakwenda shuleni na kwamba ongezeko la wanafunzi na ufaulu ni matokeo ya mafanikio ya Rais Dk. John Magufuli kutokana na kutengwa kwa fedha zaidi ya Sh Bilioni 29 kila mwezi, kwa ajili ya kufanikisha elimu bure na kati ya fedha hizo Sh bil 17.46 zinaenda kwenye elimu ya sekondari.
“Serikali imejipanga na tayari tangu Januari 7 mwaka huu, shule zote za sekondari 147 zimefunguliwa, hivyo kila mzazi ahakikishe anamuandikisha mtoto ili kuendelea na kidato cha Kwanza,” alisema Makonda na kuongeza
“Wanafunzi, wazazi na walezi wasiwe na wasiwasi kwenye hilo, kwani wanaotakiwa kwenda shule wote watakwenda.”
Wakati huo huo, Makonda amesisitiza katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa kinara kutokana na kufaulisha wanafunzi 64,861 sawa na
asilimia 92, ambapo kati ya hao wanafunzi 31,092 walikosa vyumba vya madarasa jambo liliilazimu Serikali kupambana kuhakikisha kila aliyefaulu anaendelea na masomo.
Alisema, lengo la ujenzi wa madarasa hayo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anatumia fursa ya elimu bure inayotolewa na Rais Magufuli ya kuhakikisha mtoto wa maskini anasoma ili kujikwamua kiuchumi na mwisho wa siku Taifa liwe na wataalamu wa kutosha.
Katika hatua nyingine, Makonda ametumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wanafunzi ambao watabainika kukwepa masomo, kwani watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria na hivyo wote ambao wamefaulu na wanatakiwa kuingia kidato cha kwanza waendelee na masomo.
from Jamvi La Habari http://bit.ly/2C8mkAL
