Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeamua kuwainua wakulima wa soko la Korosho, baada ya kutangaza rasmi zao hilo limepata soko la uhakika nchini Algeria huku pia ikiendelea kutafuta masoko mengine nje ya nchi.
Uamuzi huo, ulitangazwa jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda, Dk. Damas Ndumbaro,baada ya kukutana na Balozi wa Algeria hapa nchini, Saad Belabed.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Dk. Ndumbaro alisema Algeria ipo tayari kununua korosho ya Tanzania, ambapo mazungumzo ya awali yamefanyika na kilichobaki ni utekelezaji.
Alisema mazungumzo hayo ni moja ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli za kuwakomboa kiuchumi Watanzania kwa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima nje ya nchi.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zilizopo jijini Dar es Salaam.
Hivyo, alisema anaamini kuwa wakulima zao hilo, wamepata mkombozi mkubwa kwa nchi hiyo kuonyesha kuwa tayari kununua zao hilo, ambalo sasa serikali imeamua kuwasaidia wakulima.
Kwa muda mrefu, soko la korosho lilikuwa katika bara la Asia na Ulaya, hivyo kwa nchi kupata soko jipya ndani ya Afrika ni hatua kubwa na kupongezwa kwa nchi kutokana na kuwa na mipango madhubuti ya kutafuta masoko ya zao hilo.
Hivi karibuni kumekuwepo na mkakati ovu wa kusambaza uzushi, kuwa serikali haina mpango wa kuwalipa wakulima wa korosho ikiwa ni sehemu ya wapanga mkakati waliokuwa wananufaika kwa kuwanyonya wakulima wa korosho kwenye mikoa ya kusini.
Taarifa za kuaminika ilizozipata JAMVI LA HABARI zilieleza kuwa tangu serikali kuanza uhakiki wa malipo ya korosho katika mikoa inayolima korosho, wanyonyaji wa zao hilo, wamekuwa wakitumia mbinu mbali ili kuleta taharuki kwa jamii na ionekane serikali imeshindwa kuwalipa wakulima.
Mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alichukua uamuzi wa kununua korosho zote kwa sh. 3300, baada ya kukataa kuona mkulima ananyonywa, ambapo awali minada ya korosho ilikuwa ikitaka kuuza korosho kwa sh, 2500, jambo ambalo lilikuwa ni kumuumiza mkulima wa zao hilo.
JAMVI LA HABARI, limebaini kitendo hicho kinafanywa kwa ustadi mkubwa na wanyonyaji wakubwa wa korosho, wanaoitwa ‘Kangomba’, ambao kwa miaka nenda rudi wamekuwa mstari wa mbele kujinufaisha na zao la korosho kwa kuzinunua mashambani kwa kuwalaghai wakulima.
Taarifa zaidi zinasema mfumo unaofanywa na serikali wa kuhakiki utasaidia kuondoa unyonyaji wa mkulima na hata kumsaidia kupata kiasi sahihi cha malipo ya korosho, ambayo kwa muda mwingi alikuwa hapati kutokana na kiasi kikubwa kuchukuliwa na wanyonyaji hao.
JAMVI LA HABARI imebaini uhakiki unaofanywa na Wizara ya Kilimo wa shamba kwa shamba na mkulima kwa mkulima ili kuhakikisha malipo ya korosho ya sh. 3300 yanayolipwa na serikali kwa wakulima kwa ajili ya ununuzi wa korosho hizo unawafikia wakulima na mzuri japokuwa utacheleweshwa malipo kufanyika.
Serikali kupitia kwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga imesema wakulima wa Korosho wanapaswa kuamini kuwa serikali ina fedha za kutosha kuwalipa wakulima wa Korosho lakini lazima wakulima wote wahakikiwe, ili kujiridhisha kwamba anayelipwa ni mkulima wa mwisho na sio ‘Kangomba’.
Licha ya biashara ya zao la korosho kutajwa kuingiza fedha nyingi, nyuma ya pazia imebainika kuwa faida hiyo haimfikii mkulima na badala yake huishia mikononi mwa matajiri wachache huku vyama vyao vikiwa havina msaada wowote kwao licha ya vyenyewe kuingiza fedha nyingi kupitia zao hilo.
Katika uchunguzi wake, JAMVI LA HABARI limebaini njia mbili za kinyonyaji ambazo wakulima huuza mazao yao na kuendelea kufanywa maskini licha ya kupata mavuno mengi.
‘Wala maua’ na ‘Kangomba’ ni maneno maarufu katika maeneo yanayolima korosho kwani ni matajiri wanaotumia umaskini wa wakulima kulangua mazao yao kwa kununua kwa bei ya chini na kwenda kuuza kwenye minada.
Kwa upande wa ‘Wala Maua’ kama neno hilo linavyojieleza, hawa ni matajiri ambao huwafuata wakulima kuanzia mwezi wa Mei na Juni korosho zikishatoa maua na kununua korosho na kukadiria mazao kwa kuangalia maua yalivyochanua.
Jamvi la Habari limebaini kuwa mbali na mkulima kuuza korosho inagli bado ni maua hulipwa kiasi kidogo kwa kilo moja ya korosho zitakazopkadiriwa kwa shamba zima kwa kuhesabu mikorosho na kukadiria kila mkorosho unaweza kuzaa kilo ngapi.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara mmoja wa korosho kutoka mikoa ya kusini ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema wafanyabiashara wanatumia umaskini walio nao wakulima wa korosho kuwaibia kwa kuwatamanisha fedha kidogo wakati wakiwa wameishiwa.
“Mtu unaweza kujiuliza pamoja na mikoa ya kusini kuwa ndio wazalishaji wakubwa wa zao la korosho lakini wameendelea kubaki katika dimbwi la umaskini. Hii ni kwasababu wanaambulia fedha kidogo huku fedha ntyingi zikiingia kwenye mikono ya matajiri ambao huenda kuwekeza sehemu nyingine na kuuacha mkoa huo ukiwa hauna kitu,” alisema mfanyabiashara.
“Mkulima anaweza kupewa Sh. 1000 kwa kilo na kwasababu ana shida wakati huo basi huuza kwa kukadiria kwa mti mmoja unaweza kutoa kilo ngapi kisha anakupewa fedha zake na korosho zinapovunwa zinakuwa ni mali ya ‘mla maua’ hata kama zimezidi makadirio hawezi kudai chochote,” aliongeza.
Kwa upande wa ‘kagomba’ imeelezwa kuwa ni matajiri ambao hulangua korosho baada ya kuvunwa ambapo hupimwa kwa bakuli zinazokadiriwa kuwa na uzito fulani na kisha humlipa mkulima na tajiri huzipeleka kwenye vyama vya msingi na kujifanya yeye ndiye mkulima.
“Hapa ukifanyika ukaguzi utagundua kuwa asilimia kubwa ya korosho zilizopo kwenye maghala si za wakulima bali ni za matajiri ambao walinunua zikiwa shambani tena pasipo kutumia vipimo vinavyotakiwa,” alisema mfanyabiashara huyo ambaye kwa upande wake alisema hafanyi vitendo hivyo.
Muhidi Athman ni mmoja wa wakulima wa korosho wilayani Tandaimba, alisema ni kweli kuna biashara ya wala maua na kangomba ambao huvizia kipindi ambacho wakulima wameishiwa wanakwenda kununua korosho zingali maua au zikiwa shambani kwa vipimo kwa kukadiria.
Mwaka jana Tanzania ilizalisha tani 310,000 ambazo kwa wastani wa bei ya Sh 3000 kwa kilo unapata jumla ya Sh bilioni 930 ambazo zilipatikana. Mikoa ya kusini inazalisha zaidi ya asilimia 70 ya korosho yote nchi hivyo inatarajiwa fedha nyingi zingebaki katika mikoa hiyo ambayo kwa miaka mingi imekuwa nyuma kimaendeleo.
Mwaka huu jumla ya Tani 210,000 zinatarajiwa kuuzwa ambapo Rais Dk. John Magufuli ameingilia kati na kuamua kuwa serikali itanunua kwa Sh. 3300 kwa kilo baada ya mawakala wanunuzi kugoma kununua kwa bei ya zaidi ya 3000.
Hata hivyo ukweli ni kwamba fedha hizo zitakwenda kuwanufaisha zaidi Wala maua na Kangomba badala ya kwenda kuwanufaisha wakulima kama inavyodaiwa.
from Jamvi La Habari http://bit.ly/2ABglV9
Tags
News
