Waziri Lugola atoa siku 30 kwa kamishana wa uokoaji

Na Felix Mwagara, Biharamulo.

WAZIRI wa Mambo ya ndani ya nchi, Kangi Lugola amempa siku 30 Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji,Thobias Andengenye, kufanya ukaguzi taasisi mbalimbali za umma na binafsi nchini kama zina vifaa vya zimamoto.

Amesema ukaguzi huo pia ulenge zaidi katika shule za msingi, sekondari na vyuo, vituo vya kutolea huduma za afya, ili kuepukana na ajali zitokanavyo na vyanzo vya moto.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi, uliofanyika katika uwanja wa mpira mjini Biharamulo, Mkoani Kagera,jana , Lugola alisema atafuatilia utekelezaji wa agizo lake kama litakua limefanyiwa kazi jinsi anavyotaka yeye.

Pia aliwaomba Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha, wanatenga fedha za mapato ya ndani na kununua vifaa vya zimamoto katika taasisi za Serikali wanazoziongoza.

“Haiwezekani wanafunzi, wagonjwa katika zahanati mbalimbali au vituo vya afya wapate tatizo la ajali ya moto kwa kuwa tu wakurugenzi na mameneja au wakuu wa taasisi hizo wameshindwa kuweka vifaa vya zimamoto licha ya kupokea fedha za kutolea huduma,” alisema Lugola.

Aidha, Waziri Lugola alizitaka taasisi za dini kuendesha ibada kwa kuhakikisha majengo yanasajiliwa na pia Miiskiti na Makanisa yasitumike kuhifadhi wahalifu wanaotumia migongo ya kuwa wachungaji na mashekhe kama mwavuli wa maadili mema bila uzalendo.

“Makanisa na miskiti itakayobainika ina malengo hayo, sitaona haya kuifutia usajili, na pia nawataka viongozi wa dini endapo migogoro inaibuka hakikisheni mnaitatua wenyewe kwa amani,” alisema Lugola.

Katika mkutano huo Waziri Lugola, alirejea kauli yake ya kuiagiza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kupitia upya usajili na utoaji wa vitambulisho vya taifa katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili waweze kuwabaini na kuwaondoa raia wa nchi jirani zinazoizunguka mikoa hiyo.



from Jamvi La Habari http://bit.ly/2GZMGKM

Post a Comment

Previous Post Next Post