Mikakati ya DAWASA kufikisha maji Dar nzima hii hapa

Bilioni 4.5 kutengwa kila mwezi kwaajili ya uwekezaji.

NA JONAS MUSHI

SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuagiza Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), kuhakikisha maeneo yote ya mkoa huo yanafikiwa na maji, wenyewe wameelezea mikakati anayoendelea kufikisha maji maeneo ya pembezoni na yenye miinuko ambayo hayakuwahi kupata maji.

Mkoa wa Dar es Salaam ambao unakadiriwa kuwa na watu milioni 5, ni miongoni mwa majiji yaliyotajwa kukua kwa kasi barani Afrika ambapo makazi mapya yamekuwa yakichipua siku hadi siku katika maeneo ambayo hayakuwa kukaliwa na watu.

Kutokana na kupanuka huko kwa Jiji la Dar es Salaam, kumekuwepo na changamoto ya maeneo hayo kufikiwa na miundombinu ya maji umeme na barabara hasa yale ambayo hayajapangwa.

Akizungumza na jana katika mahojiano na televisheni ya Clouds kwenye kipindi cha asubuhi cha Clouds 360, Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema, tayari miradi ya kupeleka maji maeneo ya pembezoni imeanza.

Alisema yapo maeneo yaliyokuwa yamesahaulika kwa muda mrefu ambayo yalikuwa hayapati maji na sasa serikali kupitia DAWASA ikishirikiana na wadau wa maendeleo imeamua kumaliza kero ya maji katika maeneo hayo.

“Yapo maeneo yaliyokuwa yamesahaulika maeneo kama Kisukuru, Pugu, Kisarawe, Chanika haya yote tumekwishaanza miradi ya kupeleka maji maeneo hayo.

“Tutatoa maji Kibamba kwenda Kisarawe na baadae yatafika Pugu, Chanika nan a maeneo ya Minaki na pia kuna mradi wa kutoa maji Tazara. Pale Pugu tumejenga tanki kubwa la lita milioni 6 kama lile la Bagamoyo lililotembelewa na Makamu wa Rais na maji yatajazwa kwenye tanki hilo na kisha kusambazwa kwa wananchi wa maeneo hayo,” alisema Luhemeja.

Aliongeza kuwa mradi wa kutoa maji Kibamba kwenda Kisarawe umefikia asilimia 21 na unatarajiwa kufikia Juni uwe umekamilka huku ule wa kutoka Tazara bomba limefika eneo la Ukonga Magereza kuelekea Pugu.

Kwa maeneo yenye changamoto ya miinuko likiwemo eneo la Kibamba alisema tayari wamejenga matenki makubwa ya maji na mwezi huu wanakwenda kusaini mkataba wa bilioni 110 na benki ya Dunia kwaajili ya kulaza bomba kilomita 1,426 katika maeneo ya pembezoni na yenye miinuko.

“Tumejenga matenki eneo la Changanyikeni, Salasala, Bunju, Wazo na Bagamoyo na pia tumejenga matenki Kwa Msuguri, Msakuzi na Saranga yote haya yanakwenda kusambaza maji katika maeneo hayo niliyoyataja,” alisema Luhemeja.

Alisema, kinachofanyika ili kupandisha maji maeneo hayo ya miinuko, wamewekwa pampu za kuchukua maji kwenye bomba kubwa na kusukuma maji kwenda kwenye matanki ambayo yatasambazwa kwa wananchi.

Katika maelezo yake, alisisitiza wameshajenga pampu changanyikeni, salasala na wazo ambazo zinasukuma maji kwenda maeneo ya juu kwenye matanki.

Aidha, baada ya kuundwa kwa Dawasa mpya iliyounganishwa na iliyokuwa Kampuni ya Maji safi na Maji Taka (DAWASCO), imeongeza ufanisi na utendaji kazi wa Dawasa pamoja na mapato ambapo kuanzia mwaka huu imepanga kukusanya Sh. bilioni 12 kila mwaka.

Alisema katika kuhakikisha mtandao wa maji unafika kila eneo wameamua kutumia mapato ya ndani ambapo asimilia 35 ya mapato yatapelekwa kwenye miradi ya usambazaji.

“Kwa makusanyo haya ya bilioni 12 kwa mwezi tunakwenda kutenga Sh bilioni 4.5 kila mwezi kwaajili ya uwekezaji hivyo unaweza kuona jinsi ambavyo tunakwenda kusambaza maji kwa kasi sambamba na kuboresha maisha yanwafanyakazi ambapo tunatarajia kuongeza mishahara kwa asimila 40,” alisema.

Alisema kwa ujumla hali ya upatikanji wa maji kwa Dar es Salaam ni nzuri ambapo wamefikia asilimia 78 licha ya kuwepo kwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na maji na kwamba hadi 2020 maeneo yote yatakuwa yamefikiwa na maji.



from Jamvi La Habari http://bit.ly/2FjbPO4

Post a Comment

Previous Post Next Post