Na Mwandishi Wetu
HUKU mjadala juu ya muswada wa mabadiliko ya sheria za vyama vya siasa nchini ukiendelea, wanaharakati nao wameamua kuvunja ukimya na kudai wanashangaa kwanini sheria nzuri namna hii imechelewa kuletwa nchini.
Tayari baadhi ya vyama vya siasa vimeshapeleka zuio mahakamani, kutaka muswada huo usijadiliwe bungeni na kuwa sheria kwa sababu unaathiri masuala mbalimbali kwenye utaratibu mzima wa kuendesha vyama hivyo.
Kwa siku kadhaa sasa JAMVI LA HABARI limekuwa likifanya mahojiano ya mara kwa mara na watu wa kada mbalimbali ili kujua msimamo wao kuhusiana na muswada huo. Wapo walioonyesha kuridhishwa na wapo walioonyesha kutoridhishwa na uwepo wake.
Jana, baadhi ya wanaharakati walizungumza na waandishi wetu kwa nyakati mbalimbali wakidai, wanashangaa kwanini muswada huu umechelewa kuwepo kwa sababu kwa muda mrefu yapo baadhi ya mambo hayako sawa kwenye vyama vya siasa hasa vya upinzani.
Mwanaharakati wa masuala ya kijamii, Joseph Siagi alisema anashangaa kwanini muswada huo umechelewa kuletwa, kwani wapo watu walikuwa wanaumizwa na baadhi ya mienendo isiyofaa ndani ya vyama vyao.
“Kuna mambo mengi ya hovyo yaliyokuwa yanawakatisha tama wanasiasa wachaka katika vyama vya upinzani, hawakuwa na nafasi hata ya kuhoji masuala ya msingi. Wapo waliopoteza maisha na wapo waliopotea katika ramani za siasa kwa kuhoji.
“Muswada huu umeondoa ubwana mkubwa kwenye kipengele hicho, si hilo tu hata masuala ya kiongozi mmoja kukaa muda mrefu kwenye nafasi ya juu lilikuwa linawaumiza viongozi wanaochipukia,” alisema Siagi.
Siagi alisisitiza, hakuna namna yoyote njema ya kuzuia kuendelea kwa muswada huu na kujadiliwa kwa kina ili ufumbuzi upatikane.
“Kitu gani kinachowaogopesha, hawajui kama Bunge ni chombo kitakatifu ambacho hakuna jambo lolote litakalopitishwa bila kujadiliwa kwa kina na hoja zinazofaa zikatolewa kwa uhuru,” alihoji Siagi.
Katika maelezo yake, mwanaharakati huyo aliweka wazi namna Chama cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe kinavyominya vijana kuchukua nafasi nzuri kwa sababu tu kiongozi huyo amejimilikisha chama.
“Nenda kawaulize walioasisi ACT-Wazalendo watakueleza kila kitu, pale kuna ubinafsi na wapo waliojimilikisha chama akiwemo Zitto. Ndiyo maana utaona yupo mbelembele katika kupinga sheria hii. Anajua itakua na ukomo wa kuwa kiongozi wa chama.
“Kwa muda mrefu tunajua namna Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff alivyojimilikisha chama. Watu wengi wamejaribu kuchukua nafasi yake lakini wameambulia patupu. Umeona wapi mtu anagombea urais kwa miaka 30 inataka kukaribia, lakini hataki kutoa fursa kwa wengine.
“Kitu kinachonishangaza utaona watu wengi wa upinzani wanakisema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kinaminya demokrasia, wakati chama hicho ndicho kinachoongoza kwa kuwapa fursa vijana. Vilevile kila baada ya miaka 10 wanabadili mwenyekiti wa chama taifa, pamoja na viongozi wa juu wa chama kwa Zanzibar na Tanzania Bara. Lakini suala hilo limekuwa gumu kwa vyama vya upinzani ndio maana hawataki hii sheria inawabana,” alisema.
Itakumbukwa, wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya kiraia inayojihusisha na masuala ya maendeleo ya jamii ya Alliance for Development Organisation (ADOR), Habibu Mchange, alisema Muswada huo unajibu malalamiko ya muda mrefu ya wanachama wa vyama vya upinzani kwa kuondoa ukiritimba wa mtu mmoja kumiliki chama.
Alitolea mfano wa mgogoro uliowahi kutokea mwaka 2008, 2009 na 2013 ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya baadhi ya wanachama wake kuonesha nia ya kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti kwa kufuata taratibu.
“Kwa sheria tuliyonayo mtu ukiwa na mgogoro ndani ya chama ukienda kushtaki basi jua wewe si mwanachama tena lakini kwa sheria hii inayokuja mwanachama anapewa sehemu ya kukata rufaa na kupewa haki yake ndani ya chama,” alisema na kuongeza:
“Tumewahi kukandamizwa kwa kukosekana hii sheria. Mwigamba aliwahi kupigwa makofi kweye mkutano Arusha lakini hakuwa na pa kwenda kulalamika.”
Alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi wakuu wa vyama kuwatisha wanaotaka nafasi zao na hivyo kuwafanya kuendelea kubakia madarakani tena bila kupingwa wakati wa chaguzi.
“Wanalilia demokrasia lakini ndani ya vyama vyao hakujawahi kuwa na wagombea wa kuwania nafasi za juu wamekuwa wao tu tangu miaka ya tisini hadi sasa Freeman Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema, Ibrahim Lipumba ni mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif ni Katibu Mkuu wa CUF wanataka watawale hadi wafe,” alisema
Aidha, mbali ya mambo mengine faida zinazopatikana katika sheria hiyo ni udhibiti wa matumizi ya fedha za chama kwa lengo la kudhibiti na kusimamia matumizi ya fedha za zuruku ambazo ni kodi za wananchi tofauti na ilivyo sasa.
Vilevile, uzuri wa sheria hiyo tofauti na ya sasa inatoa adhabu mbadala kabla ya adhabu ya kukifuta chama kwa kushindwa kufuata sheria.
Kwa muda mrefu, kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wanacaha hasa wa vyama vya upinzani ikiwemo CUF na Chadema kuwa baadhi ya viongozi wa juu wamekuwa wakitoa fedha kwa ajili ya kuendesha chama kwa amdai wamekikopesha cham.
Mara tu fedha za ruzuku zinapoingia kwenye akaunti za chama wanazichota kwa kiwango wanachotaka wao kwa madai wanajilipa fedha walizokikopesha chama, huku ukweli wakiwa wanaujua wenyewe.
Wanachama hawana uwezo wa kujohi wala kulalamika, kwa sababu yeyote anayethubutu kufanya hivyo inakuwa ni sawa na kujifukuzisha chama.
Kwa mujibu wa hali hiyo, Siagi alisema: “Hii ni ajabu kwa sababu viongozi wa juu wa vyama vya siasa wamekuwa mstari wa mbele kupiga kelele kuwa nchi inalea mafisadi na wezi wa mali za umma, wanasema CCM haijui kulinda demokrasia kwa kufanya wizi wa kura lakini pia kuzuia maandamano.
“Lakini wao wanafanya mambo mabaya zaidi ya hayo wanayosingizia serikali na chama kinachoongoza nchi, hivyo naomba kwanza waanze kujitathmini wao ikiwa wanasema kitu kinachotoka ndani ya nafsi zao, wasiwe wanafiki.”
Ikiwa kesi itakwenda vizuri kwa upande wa serikali, ifikapo Januari 15 mwaka huu mswada kuhusu sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2018 itaanza kujadiliwa bungeni jijini Dodoma ili wabunge wakishaupitisha uwe sheria na kuanza kutekelezwa mara moja.
from Jamvi La Habari http://bit.ly/2Ff44cJ
