Breaking News

MILIONI 50 KUSHINDANIWA KATIKA SHINDANO LA STORIES OF CHANGE MSIMU NNE

Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums  Maxence Melo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa awamu ya nne ya shindano la Stories of Change.


Mkurugenzi wa Uchechemuzi wa Twaweza Annastazia Rugaba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaa kuelekea kuanza kwa awamu ya nne kwa shindano la Stories of Change

ASASI ya Kiraia ya JamiiForums yenye Makao Makuu jijini Dar es Salaam imezindua awamu ya nne (4) ya shindano la Stories of Change ambalo litaanza rasmi Mei 1, 2024 na kuiasha baada ya miezi miwili.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 19, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums  Maxence Melo amesema kauli mbiu ya shindano la mwaka huu itakuwa "Tanzania Tuitakayo" ikilenga kuhamasisha wananchi kuibua mawazo mbadala ya nini kifanyike kuipata Tanzania iliyo bora zaidi kwa kupendekeza mawazo bunifu yanayoweza kutekelezeka ndani ya miaka mitano (5), 10, 15 hadi 25 ijayo.
"Katika Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2020-2024), JamiiForums ilibuni shindano la 'Stories of Change' lililoanza mwaka 2021. Na katika awamu tatu zilizopita, takribani machapisho 6,000 yaliwasilishwa na wananchi. Miongoni mwa maudhui yaliyowasilishwa, yamechangia kuboresha mifumo ya utoaji huduma katika Sekta ya Umma na Binafsi," amesema Melo.
Melo amesema kwa shindano la mwaka huu JamiiForums itashirikiana na mashirika wake wa muda mrefu, Twaweza pamoja na wadau wengine kutoka Serikalini, asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali na makampuni binafasi katika nyanja mbalimbali kama habari, elimu, vijana, wanawake, watoto, makundi maalumu, teknolojia, afya na kadhalika.
Kwamba lengo ni kuimarisha ushiriki wa wananchi na utekelezaji wa maoni ambapo amebainisha kuwa wadau hao ndio watakaoshiriki mchakato wa kupata na kuwatuza washindi wa kisekta.
Akitaja vigezo na masharti ya kushiriki shindano hilo, Melo amesema mshiriki anatakiwa kutayarisha andiko linakoelezea Tanzania Tuitakayo lenye maono ya kibunifu ambayo yanaweza kutekelezeka ndani ya miaka mitano, 10, 15 hadi 25 ijayo katika nyanja mbalimbali mfamo elimu, afya, teknolojia, uchumi, mazingira, miundombinu na kadhalika.
Kwamba andiko liwe kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza  lenye maneno kuanzia 700 hadi 100, kadhalika matumizi ya picha, vieo na vielelezo vingine yanaruhusiwa ili kuongeza uzito wa wasilisho ambapo ikiwa picha au video zilizotumika si za mshiriki atatakiwa kutaja chanzo.
Melo ameongeza kuwa, machapisho yanatakiwa kuwa halisi na hayajawahi kuchapishwa sehemu nyingine yoyote, kwamba ubwakuzi hautaruhusiwa na kueleza kuwa maandiko yawasilishwe ndani ya miezi miwili kuanzia Mei 1, 2024 kwenye jukwaa la "Stories of Change 2024".
"Ili kushiriki, lazima mtu awe mwanachama aliyejisajili JamiiForums.com ili kuchapisha andiko lake kwenye jukwaa la shindano la "Stories of Change". Ikiwa sio mwanachama, anapaswa kujiandikisha kwa kufuata kiuongo hiki https://jamii.app/Signup," ameeleza Melo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchechemuzi wa Twaweza Annastazia Rugaba ametoa rai kwa wananchi waote wenye miaka 18 na kuendelea kushiriki katika shindano hilo ili kutimiza haki yao ya msingi ya kuchangia mawazo katika kujenga Tanzania Tuitakayo.
Amesema washindi watatangazwa kwenye jukwaa la JamiiForums "Stories of Change" na kurasa rasmi za JamiiForums katika mitandao ya kijamii na X, Facebook, Instagram, WhatsAPP na Telegram.

No comments