SERIKALI YAANIKA MAFANIKIO MKUTANO NISHATI SAFI YA KUPIKIA WA JIJINI PARIS-UFARANSA
Na ABRAHAM NTAMBATA NA TUNU BASHEMELA
MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus amebainisha mafanikio ya Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika jijini Paris Ufaransa Mei 14, 2024 na kuhudhuriwa na Mwenyekiti mwenza wa Mkutano huo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari kueleza mrejesho wa mkutano huo jana, Zuhura alibainisha baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni Pamoja na ahadi za wadau wa maendeleo na mashirika binafsi yaliyoahidi kutoa Dola za Marekani Bilioni 2.2, huku benki ya maendeleo Afrika (AfDB) ikiahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 2 kwa ajili ya Nishati Safi ya Kupikia ndani ya miaka 10.
Alitaja mafanikio mengine kuwani Nchi, Mashirika na Makampuni 130 kuidhinisha tamko la viongozi wa juu kutoa kipaumbele kwa Nishati Safi ya kupikia.
"Tamko hilo linadhihirisha nia ya kuchukua hatua kwa Pamoja na ushirikiano katika upatikanaji wa nishati afi ya kupikia," alisema Zuhura.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo alisema ajenda ya kutumia Nishati Safi ya Kupikia ni ya muhimu ili kuokoa maisha ya watu na mazingira.
Dkt. Jafo alieleza kuwa Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia umefanikiwa kwa asilimia kubwa chini ya Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika,Rais Dkt. Samia na kubainisha kuwa Uingereza imeahidi kutoa Dola za Kimarekani milioni 3.4 kwa Tanzania, ambapo ni mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo ambapo ni fursa kwa nchi katika kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua itakayowasaidia akinamama na wasichana kuzalisha na kusoma badala ya kutafuta kuni.
Waziri Jafo alisema Tanzania imejipambanua katika ajenda ya nishati safi kwa kuwa na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.
Alisema Serikali inashirikisha sekta binafsi katika ajenda ya nishati safi kuhakikisha uwezo wa wananchi katika kumudu, upatikanaji na kujenga uelewa kwa wananchi kutumia nishati safi badala ya kuni na mkaa.
Kadhalika, alisema maelekezo ya Serikali kwa taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kuacha kutumia kuni na mkaa katika kuandaa chakula ni mojawapo ya mikakati ya kuhifadhi misitu ambayo takwimu zinaonesha zaidi ya hekta laki nne zinapotea kila mwaka kutokana na ukataji wa miti.
Aidha, Dkt. Jafo alisema kuwa pamoja na mikakati hiyo pia Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti katika kila Halmashauri ambapo imeelekezwa zipande miti milioni 1.5 kila mwaka.
Aliwahimiza wananchi na taasisi kupanda miti na kuitunza kwani katika lengo la Serikali la kupanda miti milioni 266 kwa Halmashauri zote ni miti milioni 211 sawa na asilimia 76.5 ndio imestawi.
Katika hatua nyigine Zuhura alieleza kwamba pembezoni mwa Mkutano huo, Rais samia alifanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walipokutana katika Ikulu ya Elyees jijini Paris.
Kwamba masuala waliyozungumza viongozi hao ni kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika maeneo ya nishati safi ya kupikia, maji, uwezeshaji wanawake, kilimo, biashara na uwekezaji.
Mengine ni uendelezaji wa miundombinu, na kuhusu masuala ya amani na usalama Kaskazini mwa Msumbiji na Mashariki mwa Congo DR, huku viongozi hao wakikubaliana kutoa tamko linalobainisha azma ya Tanzania na Ufaransa katika kuimarisha ushirikiano kwenye sekta hizo.
No comments