Serikali yaweka msisitizo ujenzi uchumi wa kidijitali
Na Mwandishi Wetu, Arusha
*Yaguswa ubunifu Tuzo za kihistoria TEHAMA 2025
Na Mwandishi Maalumu, Arusha
JIJI la Arusha limeandika historia ya kuwa mwenyeji wa kwanza
wa Tuzo za TEHAMA Tanzania, huku Serikali ikiahidi kufanya kila linalowezekana
katika kuikuza sekta ya TEHAMA ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha nchi inakwenda
kuujenga kwa kasi uchumi wa kidigitali.
Aidha, imeahidi kuwafikia Watanzania wote, lengo likiwa
kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma katika sekta ya TEHAMA.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa aliyezindua na kutoa tuzo za TEHAMA za mwaka
2025 kwa washindi takribani 50 kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ambaye alikuwa na majukumu mengine ya
kitaifa, akimwakilisha Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alipongeza kuanzishwa kwa tuzo hizo, akisema zitasaidia
kuchochea ubunifu wa masuala ya TEHAMA na kukuza sekta ya Tehama nchini ambayo
ni muhimu katika uchumi wa kidijitali.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mara zote amekuwa akitoa
maelekezo ya kuhakikisha tunatekeleza Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa
kitaifa wa miaka kumi (10), hivyo basi, tusingependa kumuacha nyuma hata mdau
mmoja, lazima tushirikiane kuhakikisha sekta yetu ya Tehama tunaikuza,” alisema
Aliiagiza Tume ya TEHAMA kuhakikisha Tuzo hizo zinakuwa
endelevu na zinafanyika kila mwaka kwa weledi na viwango vya hali ya juu ili
kuvutia wadau zaidi kushiriki.
Tuzo hizo zilizoandaliwa na Tume ya Tehama (ICTC) kwa
kushirikiana na kampuni ya SoftVentures, Chama cha Watoa Huduma za Intaneti
Tanzania (TISPA), zilitoa fursa kwa washiriki 380 kuwasilisha kazi zao
zilizochujwa kitaalamu na kuthibitishwa na Kampuni ya Kimataifa ya Deloitte
ambayo imekuwa na jukumu la kutoa ushauri na usimamizi katika mchakato wa
tathmini ya tuzo.
Awali, akitambulisha tuzo hizo na kumkaribisha mgeni rasmi,
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema lengo la Tume
yake kutoa tuzo hizo ni kuhamasisha watu kufanya ubunifu mzuri wa masuala ya
TEHAMA nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Mohamed Abdullah alitoa wito kwa Tume ya TEHAMA kuhakikisha mwakani
mchakato wa tuzo hizo unakuwa mzuri zaidi na kushirikisha wadau wengi zaidi.
Baadhi ya washindi wa tuzo hizo akiwemo, Nafidh Ally Mola
mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kozi ya Sayansi ya Kompyuta katika Chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam na Dorice Malle kutoka Taasisi ya Mama
Mia’s Soko walisema tuzo walizopata zitawajengea hamasa zaidi katika kazi zao
za ubunifu kwa kuwa zimewapa heshima katika jamii.
Washiriki wa Tuzo za TEHAMA 2022 walichuana katika vipengele
vya Ubunifu katika Bidhaa au Huduma za TEHAMA, Matumizi Bora ya TEHAMA, TEHAMA
kwa Maendeleo ya Jamii, Kijana Aliyefanikiwa Katika TEHAMA, Wanawake Katika
TEHAMA, Usalama wa TEHAMA, Mradi wa TEHAMA wa Sekta ya Umma, TEHAMA Endelevu,
Tuzo za TISPA kwa Mtoa Huduma Bora ya Uunganishaji wa Mtandao na kadhalika.
No comments