Kamati ya Bunge yapongeza miradi ya TEHAMA, yataka wabunifu walindwe
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Maryprisca Mahundi
Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Selemani Moshi Kakoso,
imefanya ziara katika ofisi za Tume ya TEHAMA (ICTC) kwa kukagua shughuli za
taasisi hiyo, ikiwemo mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ubunifu cha TEHAMA cha
Upanga, Dar es Salaam.
Akizungumza katika ziara hiyo,
Kakoso aliipongeza Serikali na Tume ya TEHAMA kwa hatua ya ujenzi wa kituo
hicho pamoja na uanzishaji wa vituo vingine vinane vya ubunifu wa TEHAMA
vinavyoendelea kujengwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Aidha, Kamati imepongeza
kuanzishwa kwa Chuo Mahiri cha TEHAMA (DTI) kinachotarajiwa kujengwa Dodoma,
ambacho kitatoa fursa kwa vijana wengi kupata mafunzo bila kujali kiwango chao
cha elimu au kuwa na vyeti rasmi huku akisisitiza kuwa, wataalamu wa TEHAMA
watahitajika sana nchini hivyo lazima waandaliwe vyema ili kusukuma mbele
juhudi za Serikali za kutaka kuufikia kwa kasi uchumi wa kidigitali.
Ili kufikia malengo hayo, kamati
hiyo imeshauri vijana wabunifu kuendelezwa na kulindwa katika bunifu zao,
akitolea mfano kuwa, wapo vijana waliowahi kubuni vitu mbalimbali ikiwa mitambo
ya kufua umeme, helikopta na kadhalika, lakini waliishia katika changamoto
zilizowakatisha tamaa.
“Nchi inahitaji wataalamu wa kila
aina. Wenye ubunifu waendelezwe na bunifu zao zilindwe,” alisema akiwasisitiza
vijana kuchangamkia fursa za uwepo wa vituo hivyo vitakavyotoa fursa mbalimbali
kwa vijana ili waweze kujikita zaidfi katika fani zao bila ya malipo, lkini
Serikali itawapa fursa ya kujifunza zaidi, kutumia maeneo ya vituo kama ofisi
zao na pia furs ana kupikwa kibiashara, kisheria na kadhalika waweze kumudu
kujiajiri na kusimamia shughuli zao.
Kamati hiyo pia ilishauri
kuandaliwa kwa Sera na Sheria zitakazowalinda wabunifu wa TEHAMA, ikizingatiwa
kuwa kumekuwa na changamoto za wabunifu wengi kushindwa kufanikisha bunifu zao
au hata kuzuiliwa kuziendeleza.
Kakoso aliongeza kuwa Tanzania
inalenga kuwa jamii isiyotegemea fedha taslimu (cashless society), hivyo kuna
haja ya kuwa na wabunifu wengi wa TEHAMA watakaobuni mifumo ya kidijitali
inayohitajika.
Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Maryprisca Mahundi, alisisitiza kuwa wizara yake inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha bunifu za vijana zinakuwa na tija.
“Vijana wengi wa Tanzania ni
wabunifu na wamekuwa wakitengeneza bunifu mbalimbali, lakini wamekuwa wakifanya
kazi kiholela. Sasa tunakwenda kurasimisha bunifu zao ili ziwe halali na ziwe
na manufaa,” alisema Naibu Waziri Mahundi.
Kituo Kikuu cha Ubunifu cha Umoja
wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU – International Telecommunication Union),
kilichopo jijini Dar es Salaam, ni moja kati ya vituo 17 duniani
vilivyoanzishwa kwa lengo la kukuza na kuunganisha wabunifu wa kidijitali
duniani kote.
Akiwasilisha taarifa yake,
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, alisema kuwa
tume hiyo inaendelea kutekeleza ujenzi wa Kituo Kikuu cha Ubunifu cha TEHAMA
jijini Dar es Salaam, huku fedha zikiwa zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa
jengo lililopo Upanga.
Dkt. Mwasaga alieleza kuwa mradi
huo unatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inahusisha ukarabati wa jengo
kuu, na unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku awamu
ya pili ikihusisha ukarabati wa majengo ya nyuma, inayofadhiliwa na Benki ya
Dunia kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (Digital Tanzania Project – DTP).
“Lengo mahususi la kutekeleza
mradi huu ni kuchochea mabadiliko ya kidijitali kwa kutumia mbinu ya kipekee ya
ekosistimu na kuimarisha uwezo wa kuendeleza ubunifu, ujasiriamali, na ukuaji
wa uchumi wa kidijitali,” alisema Dkt. Mwasaga.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga
No comments