KAMATI ZA AMANI ZINA JUKUMU MUHIMU KUHUBIRI AMANI YA NCHI – WASIRA
Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewashauri viongozi wa madhehebu ya dini wakiwemo wa kamati za amani kuhakikisha wanahubiri amani kwa Watanzania ili nchi iendelee kuwa salama.
Akizungumza jana katika hafla ya kufuturisha aliyoiandaa kwa viongozi wa dini pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu katika Mji Mdogo wa Tunduma mkoani Songwe, Wasira alisema ni vema kila mmoja akahubiri amani nchini na kwanba viongozi wa dini wanamchango mkubwa kuifanya nchi iendelee kuwa salama.
“Wahenga wanasema maendeleo bila uhuru ni utumwa na demokrasia isiyo na mipaka ni wendawezamu. Nimefurahi kumsikia Kiongozi wa kamati ya amani ya Mkoa wa Songwe umehubiri umuhimu wa amani.
“Nitoe rai kwenu kamati ya amani pamoja na viongozi wa dini wa madhehebu yote akihubiri amani, kupitia kwako kwenda kamati ya amani ambayo inahusisha madhehebu yote, tusaidieni na isaidieni nchi yenu kuzungumzia amani ili tuendelee kuwa wamoja,” alisema Wasira.
Aliongeza kuwa iwapo kamati za amani hazitafanya kazi yake vizuri basi amani inaweza ikapata mtihani kwa sababu waswahili wanasema akili ni nywele na kila mtu ana zake hivyo zinaweza kuwa ndefu au fupi lakini zote ni nywele.
“Sasa ukiamua kuzitumia unavyotaka unaweza kuiweka nchi rehani, kwahiyo vingozi wa kiroho tushirikiane kuiombea sio nchi tu lakini katika kukemea kwa sababu ndani ya madhehebu yenu wamo watu ambao pamoja na kwamba wana imani ya dini lakini wakati huo huo na shetani naye anashughulika nao…
“Naye anawashauri vinginevyo kwa hiyo mkipata nafasi ya kuwaambia lakini hiki mnachofanya ni kinyume na imani yetu kwa sababu hakuna imani ya dini ambayo haiamini kuwa mamlaka ya nchi yako kwa Mungu. Mimi ni muumini wa dini ya Kikristo lakini dini inasema kabisa kwenye Biblia mamlaka yote ya nchi yanatoka kwa Mungu na ninyi Waislamu mnapoomba dua maana yake mnamuomba Mungu aimarishe mamlaka yake hapa duniani,” alisema.
Alisisitiza kuwa, iwapo chokochoko zikitokea na viongozi wa dini wakanyamaza watakuwa wameacha kazi yao na kamati ya amani itakuwa imeshindwa kuweka nchi katika amani, hivyo ni vema wakaendelea kuhubiri amani, umoja na mshikamano.
“Nimefanya kazi na mahedhebu ya dini katika maisha yangu, miaka ile ya Jakaya Kikwete ya mwisho nilikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais ninayeshughulika na jamii pamoja na madhehebu ya dini, tulipata changamoto ya mgogoro lakini tuliipatia ufumbuzi na nchi imebaki salama,” alisema.
Alifafanua kuwa aliyaeleza hayo kwa sababu ana uzoefu kwamba suala la amani lisipoangaliwa kuna siku atatokea mtu atayumbisha Watanzana na kufanya washindwe kuelewana “ndio maana serikali pia imekuwa ikitoa rai siasa isiingizwe msikitini na kanisani, katika nyumba za ibada.”
“Wakati mwingine wanafikiri tunazuia masheikh wasigombee au wachungaji na mapadre lakini tunachosema ukiwa unaongoza dhehebu lako na wewe ni imamu wa msikiti na ndani ya msikiti kuna watu wa vyama vingi kwa hiyo ukipendelea chama chako peke yake tena kupitia msikitini utakuta mgogoro unaanzia msikitini, wanamuuliza imamu kumbe wewe chama chako ndicho hiki. Kwa hiyo mgogoro unaanzia msikitini na mgogoro unaanzia kanisani,” alifafanua.
Wasira alisema Katiba haizuii viongozi wa dini kugombea nafasi za kisiasa kama ubunge na udiwani, lakini kutumia msikiti au kanisa kuwaambia waumini wote waende hilo linaweza kusababisha mgogoro kwa kuwa ndani ya waumini wapo wafuasi wa vyama tofauti.
“Nayaeleza hayo ili tuelewane amani ya nchi yetu ni muhimu sana na Chama chetu hakitakuwa tayari kuona inaharibiwa kwa namna yoyote. Pia nitumie nafasi hii kuwaomba kamati ya amani na viongozi wa madhehebu ya dini zote tuisaidie Tanzania na tumuombee Rais wetu kwa sababu anafanya kazi kubwa. Mambo haya Mungu anaamua.
“Kuna watu wanaamini viongozi wote lazima wawe wanaume, Waislamu hivyo hivyo wanasema mwanamke hawezi kuwa imamu na kuna siku nilikwenda Mtwara wakaniambia hapa tumemchagua mwanamke lakini hawezi kuwa imamu, nikawaambia imamu sawa hawezi kuwa mwanamke lakini mbunge sio imamu na rais sio imamu.
“Hawa ni viongozi wa kiserikali lakini imamu ni kiongozi wa msikitini, kama imamu hawezi kuwa mwanamke hiyo sawa lakini kuwa kiongozi wa serikali haina tatizo. Pia kuna makabila ambayo yanasema mwanamke hawezi kuwa kiongozi lakini kabila halichagui rais.
“Rais ni wa wote halafu nchi ya wote tena kwa taarifa wanawake ndio wengi. Sisi wanaume tunashinda kwa huruma tu wangetunyima tungepata shida. Wanawake nchini wako asilimia 52 , hivyo ni wengi kuliko wanaume.”
Awali Sheikh Nassoro Abdallah wa Mji Mdogo wa Tunduma alitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kuendelea kuiombea nchi na viongozi wake iendelee kuwa yenye amani.
== ==
No comments